The House of Favourite Newspapers

Kamanda Sirro: Hatutaruhusu Mahasimu wa CUF Kukutana Buguruni (+VIDEO)

0

JESHI la Polisi Kanda Maalum, Dar es Salaam, limeikataa barua ya Mbunge wa Temeke, Abdalah Mtolea, iliyokuwa inaomba wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwenda kufanya usafi wa mazingira katika ofisi ya chama hicho iliyopo Buguruni, Aprili 30 mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu barua hiyo aliyoipokea Aprili 27 mwaka huu, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Saalaam, Simon Sirro, amesema kuwa wameamua kupiga marufuku zoezi hilo kutokana na sababu za kiusalama kuhusiana na mgogoro wa muda mrefu unaoendelea ndani ya chama hicho.

Badala yake wameshauriwa kila mwanachama wa CUF au mwananchi yeyote afanye usafi katika eneo lake analoishi au ofisi yake anayofanyia kazi na kwamba kitendo hicho cha wanachama hao kukusanyika kutoka maeneo mbalimbali kwa kigezo cha kufanya usafi kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Kamishna, Sirro akionyesha baadhi ya madumu yenye pombe haramu ya gongo nayo yaliyokamatwa kwa wanahabari.

 

Wakati huohuo, Kamishna Sirro amesema Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho kwa upande wa Lipumba, Abdul Kambaya na wengine sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kutokana na vurugu zilizofanyika wiki iliyopita katika mkutano uliofanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulikuwa ukifanywa na wanachama wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Sharrif Hamad.

Alieleza pia kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi, Sura Namba 322 Mapitio ya 2002 na PGO. 403(1) b na C, mkusanyiko huo umezuiwa, hivyo wametakiwa kufuata maelekezo hayo.

Wakati huohuo, mtuhumiwa sugu wa wizi wa magari jijini Dar es Salaam, John Maangisi, alikamatwa Aprili 20 na jeshi la polisi akiwa na magari matano nyumbani kwake yaliyodaiwa kuwa ya wizi maeneo ya Mbezi-Msakuzi Machimbo ambapo jeshi hilo limesema mtuhumiwa huyo amekuwa akijihusisha na wizi wa magari katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Magari yaliyokamatwa ni T10 DCY aina ya Toyota Noah rangi ya fedha (Silver), T674 CCD aina ya Nissan Murano rangi nyeusi na T203 BTZ aina ya Toyota Prado rangi nyeusi na magari mengine mawili ambayo hayana namba.

Na Denis Mtima/GPL

Leave A Reply