The House of Favourite Newspapers

Prof. Assad Adai Asilimia 60 ya Viongozi Serikalini Hawana Uwezo

0

Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,  Profesa Mussa Assad amesema kuna haja ya kuanza na safu mpya  ya viongozi serikalini,  kwa kile alichokidai kuwa waliopo  wengi hawana uwezo mzuri kiutendaji.

 

 

Profesa Assad amesema hayo leo Aprili 20, 2021 wakati wa uzinduzi wa mfululizo wa midahalo kwa umma itakayokuwa ikiandaliwa na Chuo Kikuu cha Waislamu cha  Morogoro (MUM).

 

 

Amesema kwa mtazamo wake asilimia 60 au 50 ya viongozi ndani ya Serikali sio wazuri, hivyo  wanapaswa kupumzishwa ili mambo yaanze upya.

 

 

“Viongozi wengi sio wazuri au hawakidhi kiwango kinachohitajika, tatizo langu ni moja tu inapofika mahali unaona mtu anakosea na huwezi kusema kama mtu anakosea, unakuwa umefika mahali pabaya sana,” alisema Profesa Assad na kuongeza:

 

 

“Sio lazima umkosoe wazi wazi,  lakini angalau basi andika kwamba mheshimiwa nimeona umefanya jambo hili na hili, lakini nafikiri kimsingi jambo hilo halikuwa sawa;  rai yangu turekebishe hapa na hapa, akipata rai kwa mtu mmoja atakasirika, akipata rai hiyo kwa watu 10 kwenye cabinet (baraza) yake lazima asikilize.”

 

 

Amesema tatizo ni kwamba watu wote wamekuwa waoga;  imefika mahali watu wengine wananyamaza tu. “Ndiyo maana nasema tuanze upya tuanze na hao wachache ambao wanakwenda vizuri, hilo pia ni somo kwamba ambao nao ‘in the future’ (baadaye) watakuwa wa ovyoovyo, dawa yao ni hiyo ya  kuwaweka kando na kuanza upya,” amesema.

Leave A Reply