MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema katika msimu huu wa maonesho ya 44 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam unatoa huduma kamili kama ambazo zinazopatikana kwenye ofisi zake kote nchini.
Akizungumza kwenye banda namba 13 la Mfuko huo kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu kama Sabasaba, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF Bw. Abdul Njaidi amesema kwa mantiki hiyo Mfuko umewaalika wanachama wa Mfuko na wananchi kwa ujumla kufika katika banda hilo ili kujipatia huduma na taarifa mbalimbali.
“Tunawakaribisha wanachama wetu na wananchi kwa ujumla kutembeela banda letu kwani huduma zote za kiofisi ambazo zinapatikana kwenye ofisi zetu zilizoenea kote nchini zinapatikana hapa.” Alisema Abdul Njaidi.
Alitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na mwanachama kupata taarifa kuhusu Pensheni, Mafao, uhakiki, uwekezaji na taarifa za michango.
Katika hatua nyingine, Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Uendelezaji Bishara Tanzania (TANTRADE), Theresa Chilambo amesema Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuyafungua rasmi maonesho hayo Ijumaa Julai 3, 2020.