The House of Favourite Newspapers

Rais Akwaa Skendo ya Kuchepuka

0

RAIS aliyeko madarakani wa Ghana, William Addo Dankwa Akufo-Addo amekwaa skendo nzito akidaiwa kuchepuka na mwanamama Serwaa Broni.

 

Skendo hiyo imekuwa ya moto mno kwenye vyombo vya habari vya kimataifa baada ya mwanamama huyo mwenye watoto wanne kusambaza picha kadhaa mitandaoni zikimuonesha akila bata na mtu anayefanana na Rais Akufo- Addo wa Ghana.

 

Akufo-Addo aliingia kwenye kiti cha Urais tangu mwaka 2017 na baadaye mwaka 2020 alichaguliwa tena kutumikia kiti hicho cha Rais ambacho kitafikia ukomo wake mwaka 2025.

 

Akufo amezaliwa Machi 29, 1944 hivyo hadi sasa ana umri wa miaka 77. Mitandao mikubwa nchini Ghana imeripoti juu ya habari inayomuhusu Rais Akufo-Addo kuchepuka na mwanamama Serwaa Broni kufuatia picha zinazosambaa mitandaoni za wawili hao.

 

Katikati ya wiki iliyopita, Serwaa Broni aliposti video mitandaoni akieleza namna Rais huyo wa Ghana alivyomtaka kimapenzi na kusababisha kutishiwa usalama wake baada ya watu wanaosemekana ni maofisa wa usalama waliotumwa na Rais, kumuandama wakimshinikiza azifute video na picha alizonazo zinazomuonesha yeye na Rais wakiwa pamoja.

 

Kulingana na maelezo ya mwanamama huyo, Rais Addo alianza kujuana naye tangu mwaka 2016 wakati bado hajawa Rais wa Ghana.

 

Kwa mara ya kwanza walikutana nchini Canada ambapo walizungumza mengi na kujuana kwa undani, wakati huo Rais Addo akionesha dhamira yake ya kumuhitaji kimapenzi mwanamama Serwaa Broni.

 

Inadaiwa kwamba, mara nyingi Rais Addo alikuwa akilazimisha kuonana na mwanamama huyo, huku akituma ndege na pesa za malazi ili iwe rahisi kwa wawili hao kukutana.

 

Serwaa Broni ameeleza kuwa, kwa muda ambao alikuwepo nchini Ghana, basi Rais Addo alikuwa akimuhitaji kila dakika wawe pamoja.

 

Naam! Unaweza kusema ng’ombe hazeeki maini kwani habari za wawili hao kuwa pamoja zilianza tangu mwaka 2017, lakini siku chache zilizopita habari hizi zimeibuka kwa kasi nchini Ghana huku zikiacha mshangao kwa watu wa karibu wa Rais Akufo-Addo.

 

Mwanamama Serwaa Broni alinukuliwa akisema kuwa, maisha yake yapo hatarini na anaishi kwa msongo mkubwa baada ya Rais Addo kufanya kila mbinu za kumdhuru na kuharibu ushahidi wote alionao zikiwemo picha na video zinazowaonesha wawili hao wakiwa pamoja.

 

Hakuna picha wala video inayowaonesha wawili hao wakiwa faragha, lakini picha na video zinazosambaa zinawaonesha wawili hao wakiwa pamoja, wakizungumza na nyingine wakiwa wanatembea.

 

Mwanamama Serwaa Broni anathibitisha kupigiwa simu na Rais Addo muda mfupi tu baada ya kuposti picha na video katika Mtandao wa Facebook ambapo Rais Addo alimsisitiza na kumuomba mwanamama huyo azitoe picha na video zote alizoweka mitandaoni kwa kile alichodai kwamba zitamdhoofisha kisiasa.

 

Licha ya skendo hiyo kuzagaa hata katika vyombo vya habari vya kimataifa, lakini Rais Addo hajalizungumzia suala hilo sehemu yoyote.

Imeandikwa na Bakari Mahundu kwa msaada wa mtandao.

Leave A Reply