The House of Favourite Newspapers

Rais Amfuta Kazi Waziri Mkuu, Asimamisha Bunge kwa Siku 30

0
Hichem Mechichi aliyesimamishwa kazi.

Rais wa Tunisia, Kais Saied amemfuta kazi waziri mkuu wake, Hichem Mechichi na kusitisha shughuli zote za bunge kwa muda wa siku 30, kufuatia maandamano makubwa ya wananchi yaliyotokea Jumapili, Julai 26, 2021.

 

Katika maandamano hayo yaliyokuja baada ya miezi kadhaa ya kulegalega kwa hali ya utulivu na usalama nchini Tunisia, wananchi wenye hasira waliingia mitaani, kuonesha hasira zao kwa serikali juu ya namna ilivyoshughulikia vibaya suala la Covid 19.

 

Rais Saied akilihutubia taifa Jumapili mara baada ya kumalizika kwa kikao chake cha dharura na wakuu wa vyombo vya usalama, amesema ameamua kuchukua uamuzi huo mgumu ili kurejesha hali ya utulivu nchini Tunisia na kueleza kwamba atashirikiana na waziri mkuu mpya atakayeteuliwa baadaye kutuliza hasira za wananchi.

 

Maandamano ya Watunisia, yamekuja wakati taifa hilo likiadhimisha siku ya uhuru wake ambapo tofauti na miaka mingine, mwaka huu nchi hiyo imekumbwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona, jambo linaloonesha kuwakasirisha mno wananchi hao.

 

Polisi katika Mji Mkuu wa Tunis, walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wakishinikiza kuvunjwa kwa bunge la nchi hiyo huku wengine wengi wakikamatwa na kuwekwa mahabusu.

 

Hasira za wananchi zinatokana na marufuku za kutotoka nje zilizopitishwa na bunge la nchi hiyo ili kupambana na maambukizi ya Corona, ambapo wamelalamikia kwamba marufuku hizo zimezidi kufanya hali za wananchi kuwa mbaya kiuchumi.

 

Licha ya wapinzani nchini humo kukosoa uamuzi wa rais huyo kumtimua waziri mkuu wake, Rais Saied amejitetea kwa kusema hajavunja katiba na kwamba sheria zinamruhusu kuchukua uamuzi kama huo, inapotokea usalama wa nchi ukawa mashakani.

 

Akaongeza kwa kuwaonya watu wote na vikundi vya waasi ambavyo vinataka kutumia machafuko hayo kama sehemu ya kufanya uhalifu kwamba jeshi la nchi hiyo litakuwa makini kukabiliana nao ipasavyo.

 

Leave A Reply