The House of Favourite Newspapers

Rais Ateua Tume Mpya ya Uchaguzi Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, leo Juni 20, 2018 amemteua Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid kuwa Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

 

Katika taarifa iliyotolewa leo Juni 20, 2018 na Ofisi ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee, imesema Rais Dkt. Shein, amefanya uteuzi huo chini ya kifungu 119 cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

 

Pamoja na hayo Rais Dkt. Shein amefanya uteuzi wa wajumbe wengine sita wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambao ni Mabruki Jabu Makame, Feteh Saad Mgeni na Makame Juma Pandu, wengine ni Dkt. Kombo Khamis Hassan, Jaji Khamis Ramadhani Abdula na Bi Jokha Khamis Makame.

 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa wajumbe wote walioteuliwa wanatakiwa kufika Ikulu ya Zanzibar, Ijumaa Juni 22, 2018 saa 4:00 asubuhi kwaajili ya kuapishwa.

 

April 18, 2018 aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha alitangaza kustaafu baada ya kumaliza muda wake kama mwenyekiti wa tume hiyo baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitano tangu April 30, 2013.

Comments are closed.