The House of Favourite Newspapers

Waliokula Nyama ya Kiboko Hatarini… Dokta Afunguka!

 MOROGORO: Ilikuwa ni patashika nguo kuchanika! Wananchi wa Kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro mjini, wamekumbwa na taharuki baada ya kiboko kuibuka nchi kavu na kuvamia makazi ya watu, kisha kuuawa na nyama yake kugawiwa kwa watu, tukio lililotokea jirani na Makaburi ya Kanisa la Mtakatifu Monica, Risasi Mchanganyiko linakusimulia mwanzo mwisho.

 

Daktari wa mifugo, Onesmo John aliyezungumza na gazeti hili baada ya tukio hilo alisema kwamba, kula nyama ya mnyama yoyote bila kupimwa ni hatari kwa afya ya walaji.

Daktari huyo alionya kwamba watu wanaoshika na kula nyama ya wanyamapori isiyopimwa wanaweza kuambukizwa magonjwa hatari kama vile kimeta, ebola pia virusi vinavyofanana na Ukimwi.

“Kimeta ndio ambao umewahi kulipuka hapa nchini, ni ugonjwa wa wanyama unaoambukiza sana hata binadamu, humfanya mnyama kuwa na homa kali na pia wengu na koo lake kuvimba, mtu anaweza kuambukizwa akila nyama ya mnyama auguaye ugonjwa huo.

 

“Kwa maana hiyo wale watu wa Morogoro waligombea ile nyama ya yule kiboko wako hatarini kama hajapimwa baada ya kuuawa kwani madhara yake ni kama nilivyoeleza hapo awali,” alisema daktari huyo.

 

Katika tukio hilo la juzi Jumatatu, mara baada ya wananchi wa eneo la Kihonda kumshuhudia mnyama huyo aliyekadiriwa kuwa na uzito wa kilo 2,000 akirandaranda mtaani kwao, walipeana taarifa na kukusanyika sehemu moja.

“Tulianza kumuona akiwa kwenye kadimbwi kadogo ka’ maji, baadaye akaanza kurandaranda mitaani ndipo alipozua taharuki na watu kuanza kukimbia hovyo,” alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Ali Juma.

 

Shuhuda huyo alisema, baada ya kuona kiboko huyo anaweza kuleta madhara kwa wananchi, waliamua kutoa taarifa kwa uongozi wa kata ambao nao ulitoa taarifa Polisi na kwa uongozi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambao walifika ndani ya muda mfupi eneo la tukio.

“Baada ya kuona mnyama huyo anaweza kuwadhuru watu, askari wa jeshi la wanyamapori waliamua kumuua kwa kumtandika risasi kichwani,” alisema Juma.

Mara baada ya askari wa wanyamapori kumuua, umati wa watu uliokuwa na visu, mashoka na mapanga ulivamia na kutaka kuanza kugombea nyama ya mnyama huyo ndipo askari wa wanyamapori walipolazimika kupiga risasi za moto hewani kuwatawanya.

 

Baadaye askari hao wa wanyamapori walichukua kichwa cha kiboko huyo wakidai ni nyara ya serikali kisha wakamburuza mnyama huyo kwa kumvuta na gari hadi Ofisi ya Kata ya Kihonda ambayo haikuwa mbali na eneo la tukio.

Walipofika katika ofisi hiyo, walimcharanga kiboko huyo na kugawa nyama kwa wananchi waliokuwa wamezingira ofisi hiyo.

Hata hivyo, kuna madai kwamba, nyama hiyo haikupimwa na daktari wa wanyama kuona kama haina madhara kwa walaji. Akizungumza na gazeti hili, ofisa mwandamizi wa wanyamapori, mamlaka ya wanyamapori, Privatus Kasisi alisema walilazimika kumpiga risasi hadi kufa mnyama huyo ili asilete madhara kwa wananchi.

 

Naye Diwani wa Kata ya Kihonda, Gabriel Temu aliyekuwepo eneo la tukio alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema anashukuru kwamba halikuleta madhara yoyote kwa wananchi na akawashukuru mamlaka ya wanayapori pamoja na polisi kwa ushirikiano walioutoa kwa haraka na kuweza kumdhibiti kiboko huyo ambaye angeweza kusababisha maafa.

STORI: Dunstan Shekidele, Risasi Mchanganyiko.

Comments are closed.