The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli; ‘Huu ndiyo unyama alioufanya mchina bila kufanywa chochote’

0

MCHINA MAUAJI GEITA (1)Stori: Mwandishi Wetu, Wikienda

GEITA: “Uhusiano wa Tanzania na China ni wa miaka mingi iliyopita, tangu enzi za mwasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na mwenzake wa taifa hilo, hayati Mao Tse Tung, lakini baadhi ya raia wa nchi hiyo ambao siyo waadilifu, wamekuwa wakitaka kuchafua urafiki wetu kwa kufanya matukio ya ajabu,” anaanza kusema Michael Kusekwa, mkazi wa Geita.

MCHINA MAUAJI GEITA (2)Kusekwa aliyasema hayo, Jumamosi iliyopita kufuatia tukio la kijana aliyejulikana kwa jina moja la Elisha, mkazi wa Kabimbi mkoani hapa kufariki dunia, Ijumaa iliyopita akiwa njiani kupelekwa hospitali kwa madai ya kuanguka mgodini baada ya kulazimishwa kuingia kufanya kazi na mmoja wa Wachina anayefanya kazi kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Nyamahona uliopo Kijiji cha Nyamahona.

Ilidaiwa kuwa, awali kijana huyo na wenzake walitaka nyongeza ya mshahara kwanza lakini bosi wao wa Kichina aliwalazimisha kuingiza kazini na ndipo likatokea tukio la kuanguka.

MCHINA MAUAJI GEITA (3)ILIVYOCHUKULIWA

Kufuatia madai hayo, mitandao mbalimbali Bongo imeandika habari hiyo ikisema; ‘Mchina amuua mfanyakazi wake kwa kipigo’ huku wakitupia picha inayomwonesha raia mmoja wa China akimpa kichapo Mbongo huku ikidaiwa kuwa, ndiyo ya tukio hilo.

ANAVYOJUA KUSEKWA

Kwa mujibu wa Kusekwa, picha hiyo inayomwonesha kijana huyo akipigwa na Mchina siyo ya marehemu Elisha, bali ni tukio lililojiri pia kwenye moja ya migodi ya Geita siku kadhaa nyuma.

“Kwanza naomba niseme kuwa, picha ya kwenye mitandao kwamba ni Mchina anamtesa Elisha siyo ya kweli. Yule ni kijana mmoja, sijajua wa wapi, alipigwa na Mchina mmoja siku kadhaa nyuma akidaiwa kuiba madini mgodini,” alisema Kusekwa.

Akaendelea: “Ila ninachotaka kusema ni kwamba, pamoja na yote, bado iko haja ya rais wetu, Dk. John Pombe Magufuli kufuatilia kwa kina sifa za raia wa kigeni kuingia nchini. Wapo wengine si waadilifu wanawaharibia wenzao.

KUHUSU WACHINA

“Mimi kwangu Wachina ni ndugu zangu. Ila, baadhi yao siyo waadilifu kabisa. Mimi namwambia Rais Magufuli, aangalie mfano kwa huu unyama alioufanya huyo Mchina wa kumtesa kijana kwa madai aliiba madini halafu akaachwa bila kufanywa chochote, si sawa. Asingechukua sheria mkononi, kama aliiba kwa nini asingempeleka polisi?

INGEKUWA KWAO CHINA

“Mimi ninavyowajua Wachina, ingekuwa kwao, Mbongo amefanya unyanyasaji ule, asingepona. Hapa namaanisha angechukuliwa hatua kali za kisheria, hata kurejeshwa nchini. Nao wao wakifanya hivyo kwetu iwe hivyo, wasiachwe tu maana hawa ni wale wanaochafua sifa nzuri za wenzao wema.”

TUKIO LA KIJANA ELISHA

Juzi, Wikienda lilifunga safari hadi Kijiji cha Nyamahona na kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi aliyewahi kufanya kazi na marehemu Elisha ambapo alisema:

“Siku ya kifo cha Elisha ilikuwa hivi; Wachina wameingia mkataba wa kuchimba madini kwenye eneo la Bole kwa miaka mitano, wanatulipa elfu kumi na tano (15,000) kwa zaidi ya saa 12, tukijaribu kuomba kuongezewa mshahara wanatupiga na kutulazimisha kufanya kazi kwa nguvu.

“Kazi ya maduara (shimoni) ni ngumu sana kwani kuna maduara mengine yana urefu wa viwanja 2 vya mpira wa miguu na kuendelea, ukiingia duarani ni kama umeingia kuzimu.

“Ijumaa marehemu Elisha na wengine waligoma kwa madai ya kuongezewa mshahara, lakini wakalazimishwa kuingia. Muda wa kutoka ulipofika, ndipo Elisha akaangukia humo duarani.

“Alipotolewa nje alikuwa akipumua kwa mbali huku akitokwa na damu na vitu vyeupe ambavyo sikuvifahamu.

“Baada ya kukaguliwa pale na kutafutiwa usafiri kwa ajili ya kupelekwa Hospitali ya Geita kwa matibabu, Elisha alifia njiani,” alisema mfanyakazi huyo.

MENEJA WA MGODI

Gazeti hili lilipotafuta meneja wa mgodi ambaye alifahamika kwa jina moja la Kulwa hakupatikana kwani alikuwa amechukuliwa na polisi muda mchache baada ya gazeti hili kuwasili eneo la tukio.

WACHINA WENYEWE

Hata hivyo, juhudi za kuwapata Wachina hao kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kwa kukataa na kuwa wakali hata kuwasogelea.

Kabalo Malemi ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamahona, yeye amekiri kutokea kwa tukio hilo na alisikitishwa kwa kitendo cha ndugu wa marehemu kumkataa yeye (mwenyekiti) kushiriki msiba huo kwa namna yoyote kwenye tukio hilo huku kukiwa na madai kuwa, ndugu hao walipewa shilingi laki sita ili kumaliza suala hilo.

MCHINA KUMTESA MBONGO

Wikienda lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Mponjoli Mwabulambo ili azungumzie matukio hayo mawili, la Elisha kudaiwa kufa kwa kulazimishwa kuingia mduarani na kuanguka na la mwingine kuteswa siku za nyuma, alisema:

“Mimi nipo safarini, siko Geita. Kama mna mwandishi pale, mwambieni aende ofisini ataambiwa kila kitu,” alisema Kamanda Mponjoli.

WIKIENDA NA MNADHIMU WA POLISI

Baada ya kuzungumza na Mponjoli, Wikienda lilizungumza kwa njia ya simu na kamanda mmoja wa polisi ambaye alitajwa kuwa msaidizi wa Kamanda Mponjoli ambaye alisema:

“Kwanza nataka kusema kuwa, picha zinazozagaa mtandaoni si za tukio la Ijumaa (iliyopita). Zile ni picha za zamani. Kuna kijana mmoja kwenye mgodi alidaiwa kuiba mawe (madini), ndiyo yule bwana unayemwona kwenye picha akamfanyia vile.”

Wikienda: “Kwa hiyo si Elisha anayedaiwa kufariki dunia Ijumaa?”

Kamanda: “Siyo yeye.”

Wikienda: “Sasa yule mlimchukulia hatua gani kwa ukatili ule?”

Kamanda: “Hakuna hatua, kwani alichotakiwa kufanya yeye baada ya kuteswa vile ni kwenda kufungua malalamiko polisi. Sasa yeye alipoachiwa, aliamua kurudi kwao, Bariadi (Shinyanga).”

KUHUSU ELISHA

Wikienda: “Vipi kuhusu Elisha anayedaiwa kuwa alipigwa?”

Kamanda: “Ninavyojua mimi Elisha alianguka mgodini wakati akitoka nje, akaumia. Wakati akipelekwa hospitalini kupatiwa matibabu alifariki dunia.”

Hata hivyo, kamanda huyo aligoma kutaja jina lake akidai atalitaja atakapotoa taarifa kamili kwa vile alizotoa kwa gazeti hili ni za awali.

“Jina nitalitaja baadaye kwenye taarifa kamili. Kwa sasa, RCO (Afisa Upelelezi wa Mkoa), OC-CID (Afisa Upelelezi wa Wilaya) wamekwenda mgodini kufuatilia suala hilo,” alisema kamanda huyo.

WACHINA WASIO WAADILIFU

Usiku wa Septemba 4, 2014, Wachina wanaochimba njia ya mabomba ya gesi mikoa ya kusini walidaiwa kumuua mtu aliyesemekama ni mwizi ambaye ni mzawa wa Kijiji cha Ikwiriri, Rufiji, Pwani.

Januari 16, mwaka huu, gazeti moja la kila siku nchini, liliandika habari ya Mchina mmoja kumtwanga Mbongo hadi kupoteza fahamu.

Mchina mwingine mwezi huohuo, alitiwa mbaroni kwa madai ya kusababisha kifo cha mfanyakazi mwenzake Mbongo, Benson Msengi (28) kwa kumgonga na gari katika mradi wa maji ya Ziwa Victoria. Mchina huyo alishikiliwa na Polisi Mkoa wa Shinyanga.

Baadhi ya watu waliozungumza na Wikienda juzi, walisema kuwa, matukio ya baadhi ya Wachina kutesa hadi kuua Wabongo yasifumbiwe macho ili wale ambao ni waadilifu waishi kwenye nchi hii kwa amani na upendo.

Leave A Reply