The House of Favourite Newspapers

Rais Samia: Nisiwafiche Tozo Zitaendelea Kuwepo – Video

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa tozo za miamala ya simu zitaendelea kuwepo, na wala hataki kudanganya kuwa zitaondolewa. Amesema ukifanya kitu utasemwa, usipofanya, utasemwa, hivyo ni bora afanye, hata akisemwa, lakini wataona alichofanya.

 

Hayo yamejiri leo Alhamisi, Septemba 2, 2021 wakati Mhe. Rais aliposimama njiani katika eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam akielekea Bagamoyo kurekodi kipindi maalum cha kutangaza utalii.

 

“Tuna mambo mengi ya kufanya, tuna miradi mikubwa tulioachiwa na Rais wetu (Hayati Dkt. Magufuli) tunaendelea kuitekeleza, na ninawaahidi tutaitekeleza kama ilivyopangwa.

 

“Kuna miradi ya kijamii kama shule, barabara na hospitali tunaendelea kuitekeleza, zamani tulikuwa tunasaidiwa na wahisani lakini sasa hivi wamebadilika, badala ya misaada wanakuja tufanye biashara, tugawane faida. Katika bajeti iliyopita tuliweka tozo kwenye fedha za miamala ya simu, yamepigiwa kelele sana, nimesikia, nimekaa na wataalam tumepunguza asilimia 30 ya tozo hizo.

 

“Nataka niwaambie tozo zitaendelea kuwepo na sitaki kuwaficha. Sababu tozo zile miezi miwili tuliyoanza nayo tumekusanya kama Tsh bilioni 60 hivi, na zile zimepelekwa kujenga vituo 220 vya afya, hivyo tunajenga wenyewe.
“Tunajitegemea wenyewe ili kuweka mkono kwa wafadhiri wanaokuja na masharti yao wasituingilie mambo yetu na ndivyo tutaweza kufanya wenyewe.

 

“Mwezi Januari tutakuwa na watoto wanaoanza kidato cha kwanza na darasa la kwanza, hivyo madarasa na madawati yanahitajika, hakuna wa kutujengea ni sisi wenyewe, fedha tutakazokusanya mwezi Septemba na Oktoba, tunakwenda kujenga madarasa 500 Tanzania nzima.

“Shule mliyoomba hapa itajengwa, nitazungumza na waziri wa TAMISEMI (Ummy Mwalimu) fedha zitakazokusanywa mwezi ujao, itoke sehemu ikajenge shule watakayosomea watoto wetu, wakimbie kuvuka mabarabara wasigongwe na gari.

“Wanadamu ukifanya watasema, usipofanya watasema, bora tufanye waseme lakini wakione kuliko kutofanya kwa kuogopa maneno yao. Wanasema kelele za mlango hazimwachishi mwenye nyumba kulala sababu tumezizoea, kusemwa kupo.

 

“Maendeleo mkiyaona msichoke, tunawajengea watoto wetu wa Kitanzania na mengine tunajijengea sisi na vizazi vijavyo. Siku hizi misaada ni michache sana, mambo mengi tunafanya wenyewe, Tanzania yetu tutaijenga wenyewe. amesema Rais Samia.

Leave A Reply