The House of Favourite Newspapers

Rais Samia: Sheria ya PF3 Itazamwe Upya, Watu Wanakufa – Video

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelitaka jeshi la polisi kuangalia upya kipengele cha PF.3 kwa watu wanaopata ajali kwa sababu kinasababisha watu kupoteza maisha.

 

Rais Samia amesema hayo leo Mei 18, 2021 wakati akizindua kiwanda cha ushonaji cha jeshi la polisi kilichopo kilichopo katika Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam na kuagiza kuwa mtu anapopata ajali, kipaumbele cha kwanza kiwe ni kupatiwa matibabu, kisha hatua za kipolisi zitafuata.

 

 

“Kuna wanaopata ajali wanaumia kwa viwango tofauti tofauti mwingine anapoumia anapofika hospitali inabidi ashughulikiwe haraka, lakini sheria yetu hawezi kuhudumiwa mpaka iende PF3 watu wanafia pale hospitali, hii sheria muiangalie. Mtu akipata ajali apate huduma kwanza kisha mambo mengine yaendelee, tumepoteza watu wengi (wanafariki) sababu ya PF 3.

 

“Nimezungumza na TAKUKURU na wameweza kufuta kesi 147 ambazo waliwabambikizia watu mbalimbali huko, na nyie Jeshi la Polisi jikagueni kama mnazo za aina hiyo zifutwe. Ili tupunguze wingi wa mahabusu kule kwenye majela yetu.
“Kiwanda hiki cha ushonaji cha Jeshi la Polisi, Kurasini Dar es salaam, kitazalisha sare za Askari, nimeoneshwa uniform za awali ni nzuri mno, niviombe na Vikosi vingine vya ulinzi vije vishone hapa, tukuze zaidi Kiwanda cha Polisi,” amesema Rais Samia

 

Aidha, Rais Samia amelitaka jeshi la polisi kujielekeza zaidi kutoa elimu badala ya kutumia sheria zao kutoza faini. Pia amelitaka jeshi hilo kuwa na mfumo utakaosomeka nchi nzima na kuonesha makosa ya madereva, na yakifika kiwango fulani, dereva anyang’anywe leseni.

 

Leave A Reply