The House of Favourite Newspapers

Rais Samia: Si Siku Nzuri Kwangu, Wingu Jeusi Limetanda – Video

0

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Taifa linapita katika wakati mgumu kwani hata yeye hana furaha licha ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

 

 

Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa, Machi 19, 2021, wakati akilihutubia taifa mara baada ya kula kiapo cha kuwa Rais Tanzania Ikulu jijini Dar es Salaam kufuatia kifo cha Rais Magufuli na kwamba ametangaza kuwa na maombolezo ya siku 21.

 

 

“Nimekula kiapo nikiwa na majonzi tele na nchi ikiwa imetandwa na wingu jeusi la simanzi, nimekula kiapo katika siku ya maombolezo kwa ajili hiyo mtaniwia radhi, nitaongea kwa uchache tutatafuta wasaa mwingine hapo baadaye tuzungumze.

 

 

“Leo sio siku nzuri sana kwangu ya kuhutubia Taifa maana nina vidonda vikubwa moyoni, kiapo nilichokula leo ni tofauti na vyote nilivyowahi kula katika maisha yangu, nimekula kiapo cha juu kabisa Tanzania nikiwa na majonzi tele, mniwie radhi nitaongea kwa uchache.

 

 

“Kwa mara ya kwanza tumempoteza Rais akiwa madarakani, nichukue fursa hii kumpa pole Mama Janeth Magufuli pamoja na Mama Suzan Magufuli (Mama Mzazi wa Marehemu Dkt.John Pombe Magufuli), tunaungana nao katika kipindi hiki kigumu na kuahidi kuendelea kuwashika mkono.

 

 

“Natoa salamu za rambirambi kwa Watanzania wote kwa pigo hili kubwa ni msiba mzito ambao hatukuutarajia sote tunafahamu namna Rais Magufuli alivyoipenda nchi hii na alivyojitoa kuwatumikia watu wake, ameibadili taswira ya nchi kwa vitendo huku muda wote akimtanguliza Mungu.

 

 

“Dkt.Magufuli alikuwa Kiongozi asiyechoka kufundisha, amenifundisha mengi, amenilea na kuniandaa vya kutosha, tumepoteza Kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mpenda maendeleo na Mwanamapinduzi ya kweli.

 

 

“Nawashukuru CCM kwakuwa karibu nami tangu tulipopata msiba, nawashukuru pia Viongozi wa Vyama vya Upinzani kwa wingi wa salamu za rambirambi na kunipa pole tangu nilipotangaza msiba huu mkubwa, huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa.

 

 

“Huu ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana Upendo, Udugu wetu, kudumisha amani yetu, huu sio wakati wa kutazama yaliyopita bali kutazama yajayo, huu sio wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, ni wakati wa kufutana machozi,” amesema Rais Samia.

 

Leave A Reply