Rais wa Russia Akutana na Rais wa China Wajadili kusitisha Mapigano Ukraine
Rais wa Russia Vladimir Putin na mwenzake wa China, Xi Jinping, walitarajiwa kuijadili mapendekezo ya Beijing, kwa Russia kusitisha mapigano nchini Ukraine, wakati kiongozi huyo wa China akiwasili Jumatatu kwa ziara ya kihistoria mjini Moscow.
China imetaka kujionyesha kama nchi isiyoegemea upande wowote katika mzozo wa Ukraine, lakini Washington imeishutumu Beijing kwa kudhamiria kuiuzia silaha Moscow — madai ambayo China imekanusha vikali.
Ziara hiyo ya siku tatu ya Xi, pia inatumika kama ishara ya kumuunga mkono Putin aliyetengwa kimataifa, siku chache baada ya mahakama ya uhalifu wa kivita kutoa hati ya kukamatwa kwake kwa tuhuma za kuwateka watoto wa Ukraine kinyume cha sheria.
yombo vya habari vya serikali ya Beijing viliripoti kuwa Xi aliwasili Jumatatu mjini Moscow kwa ndege kwa ajili ya mkutano huo, ambao unatarajiwa kujumuisha mjadala wa mada yenye hoja 12 za China inayopendekeza mzozo huo usuluhishwe kwa mazungumzo, na kwa kuheshimu mipaka ya nchi zote.
Putin amekaribisha kauli ya Beijing kuhusu Ukraine kama dalili ya nia ya kuchukua “jukumu mahususi” katika kumaliza mzozo huo, huku akisema uhusiano wa China na Russia “umeimarika kwa kiwango kikubwa zaidi”.