The House of Favourite Newspapers

Rayvanny Kutoka Mtaani, WCB, Hadi Mmiliki Wa Lebo

0

RAYVVANY ni msanii aliyekuzwa na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Diamond Platnumz.Jina lake halisi ni Raymond Shaban Mwakyusa ambaye amezaliwa Agosti 22, 1994 na ni mzaliwa wa Mkoa wa Mbeya.

 

Rayvanny ni msanii, mwimbaji na mtunzi ngoma za kizazi kipya hapa Tanzania na amekuwa akiwaandikia mashairi wasanii mbalimbali wa tasnia hiyo. Rayvanny ameanza kujulikana kupitia ngoma yake ya kwanza aliyoipa jina la Kwetu.

 

Baadaye akapakua ngoma iitwayo Natafuta Kiki huku Wimbo wa Sugu ambao ukitolewa kama wimbo wa ziada kwani umechukua biti ya Bow Wow (What’s My Name).

 

Baadaye akapakua ngoma iitwayo Mbeleko, Shikwambi, Zezeta. Lakini alishishirikishwa katika ngoma iitwayo Kijuso aliyoimba na Queen Darleen.Aliwahi kuhojiwa kuhusu kujikita kwake kwenye muziki, akasema;

“Mimi nilianza kwanza kuandika, kurap kisha nikaja kuimba kwa sababu kuimba ni pamoja na kujua vizuri kupanga sauti, hilo nimejifunza kanisani, baada ya hapo ndipo nilianza kuandika ngoma za kuimba, tulikuwa watu kama sita na wote tulikwenda kanisani na walituambia kuna masuala ya kwaya, kwa hiyo siku hiyohiyo tumeingia kanisani tukaingia kwenye kwaya ya kanisa.

 

”Rayvanny anasema akiwa kanisani ndipo alipojengeka kimuziki na baadaye alikuja kushiriki katika mashindano ya Free Style wakati bado yupo shule, pia anasema kipindi anarap kwenye mashindano kuna mtu alimwambia yeye ni mzuri zaidi kwenye kuimba kuliko kuchana.

 

“Niliposhiriki mashindano ya Free Style kuna mtu alinisikia nikiimba, akasema wewe upo vizuri zaidi kwenye kuimba. Basi niliendelea kurap nikashinda kimkoa, baadaye tukashindanishwa Tanzania nzima, nikashinda, nikawa namba moja, kiukweli sikujua kama muziki una pesa hivi.

 

“Baada ya kushinda mashindano ya Free Style Tanzania nzima nikapewa mtonyo hapo ndipo niliposema haiwezekani ngoja nibadilishe staili,” anasema Rayvanny na kubainisha kuwa hapo ndipo safari yake kwenye muziki ilipokolea kwani pesa zilimfanya kuanza kuandika ngoma zake mwenyewe, zikamfanya aanze kuimbaimba hadi alipoingia chini ya usimamizi wa Tip Top Connection kabla ya kuibukia WCB.

 

Akiwa WCB, Rayvanny alishawahi kushinda Tuzo ya BET 2017 katika kipengele cha International Viewers Choice na kuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki kushinda tuzo hiyo kubwa.

 

Uzito wa jina lake uliongezeka maradufu tangu aliposhuka kwenye ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar akiwa ameshikilia mkononi tuzo yake ya BET.

 

Wakati Diamond Platnumz anachuguliwa kwa mara ya kwanza kuwania tuzo hiyo ya BET mwaka 2014 katika kipengele cha Best International Act Africa, alikuwa anafanya vizuri na ngoma yake ya My Number. Ukubwa wa ngoma hiyo ulitokana na kolabo aliyofanya na Davido ikiwa ni remix.

 

Hata alipochaguliwa kuwania tuzo hiyo kubwa duniani kwa mara ya pili mwaka 2016 katika kipengele hichohicho, bado haikuwezesha mikono ya Diamond Platnumz kuchukua Tuzo ya BET pamoja na ukubwa wa kolabo nyingine aliyofanya na Mr Flavour ya Nana.

 

Kwa Rayvanny mambo yalikuwa ni tofauti, hakuwahi kusikika katika ngoma na msanii mkubwa wa nje.

 

Mwaka huo ndipo alisikika katika kolabo na msanii kutoka Kenya, Bahati ambaye alimshirikisha Rayvanny katika ngoma yake iitwayo Nikumbushe.Rayvanny na ngoma zake tatu; yaani Kwetu, Natafuta Kiki na Zezeta aliweza kutusua na kufika kileleni Tanzania.Video zake nyingi zilikuwa zikifanyika hapa nchini na siyo nje.

 

Video yake ya Kwetu ilifanyika hapa Bongo ikiongozwa na Godfather, video yake ya pili ya Natafuta Kiki pia ilifanyika Bongo chini ya Kwetu Studio.

 

Ngoma hizo mbili ndizo zimempa Rayvanny umaarufu mkubwa na kujulikana ndani na nje ya nchi, lakini hakukwea pipa hadi Afrika Kusini kutengeneza video zake huko kama wasanii wengi wanavyoamini kufanya hivyo ni njia ya kutusua kimataifa.

 

Kwa sasa Rayvanny yawezekana ni miongoni mwa ya wasanii wenye mkwanja mkubwa hapa Bongo.Kufanya kolabo nyingi pamoja na kutoa hit kibao yawezekana ndiyo sababu kubwa iliyomfanya aweze kuwa na wafuasi wengi katika mitandao yake ya Instagram, Facebook pamoja na YouTube.

 

Rayvanny ni miongoni mwa wasanii waliobahatika kupata mtoto kutoka kwa mpenzi wake, Fahyvanny ambaye alijizima data na kuamua kubadilisha dini yake ya Kiislam na kuwa Mkristo, kisa mapenzi. Kabla ya kusainiwa Wasafi, Rayvanny alikuwa anawasiliana na Meneja wa Diamond Platnumz, Babu Tale ambaye kuna wakati anasema Tale aliona kama ni usumbufu, lakini yeye alikuwa hakati tamaa.

 

Anasema baadaye Tale aliamua kumchukua na kumuweka kwenye Kundi la Tip Top pamoja na Dogo Janja.Diamond Platnumz ndiye mtu wa kwanza kugundua kipaji cha kuimba cha Rayvanny hivyo akaona amchukue na kumsainisha kwenye lebo yake ya WCB na kuwa msanii wa pili kujiunga na lebo hiyo baada ya Harmonize.

 

Leo hii Rayvanny ni kiungo mzuri sana na mwenye mchango mkubwa ndani ya lebo hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupanga mashairi na kuwa na sauti tamu ya kusikilizika masikioni.Hata hivyo, Rayvanny ameanzisha lebo yake inayoitwa Next Level Music kama alivyofanya Harmonize kuanzisha Konde Gang Music Worldwide.

MAKALA: ELVAN STAMBULI

Leave A Reply