The House of Favourite Newspapers

RC Chalamila: Bora Kuwepo Chama Kimoja cha ‘Magufuli Ruling Party’ – Video

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila,  amesema kuwa haoni sababu ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini badala yake kuwe na chama kimoja tu kitakachoitwa ‘Magufuli Ruling Party’.

 

Chalamila ameyasema hayo leo Jumanne, Aprili 30, 2019, wakati akitoa salamu za mkoa wake kwa Rais John Magufuli kwenye mkutano wake na wananchi wa Wilaya ya Kyela aliposema hayo ni kutokana na mambo mengi mazuri ya kimaendeleo ambayo Magufuli ameyafanya kwa kipindi cha miaka mitatu akiwa madarakani.

 

“Mheshimiwa Rais umefanya mengi sana mema kwa nchi yetu, umetoa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, hapa Kyela umetupatia vitambulisho 10,000, wananchi 8,850 wameshagawiwa vitambulisho hivyo kwa gharama ya shilingi 20,000 kwa kila kitambulisho.

 

“Katika suala la elimu bure, katika mkoa wa Mbeya unawalipia wanafunzi wa shule za msingi zaidi ya 400,000 na wa sekondari zaidi ya 86,000.  Tunakushukuru sana mheshimiwa rais. Katika mazuri haya unayoyafanya, sioni kama kuna haja ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa, badala yake kuwe na chama kimoja tu kinachoitwa ‘Magufuli Ruling Party’, amesema Chalamila.

 

Hata hivyo, Magufuli alimjibu Chalamila na kusema hakubaliani na wazo lake kwa sababu yeye anapenda mfumo wa vyama vingi, sababu vipo kwa mujibu wa katiba, vinaleta changamoto na kuongeza upinzani, lakini akaongeza kuwa licha ya kuwa na vyama vingi anatamani Chama Cha Mapinduzi ndiyo kiwe kinashinda.

VIDEO: MSIKIE CHALAMILA AKIFUNGUKA

Comments are closed.