The House of Favourite Newspapers

Refa Aliyeipa Simba Bao Afungiwa Miaka Mitatu

0

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imechukua maamuzi ya kutoa adhabu kali kwa mwamuzi namba mbili Kassim Safisha aliyezua utata katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, Simba dhidi ya Namungo FC, ambapo amefungiwa kuchezesha soka kwa miaka mitatu. Taarifa iliyotolewa na bodi hiyo

 

imeeleza kuwa sababu kubwa ya maamuzi hayo ni kushindwa kutafsiri sheria ya kuotea katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 29, 2020 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambapo straika wa Simba, Meddie Kagere alifunga bao la tatu akionekana kuwa ameotea katika ushindi wa mabao 3-2. Taarifa iliyotolewa jana na TPLB imeeleza Safisha amefungiwa miaka mitatu kwa mujibu wa Kanuni namba 39 (1) (a) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

ADHABU NYINGINE: Mchezo wa Azam FC dhidi ya Mtibwa, mwamuzi Meshack Suda ameandikiwa barua ya kukumbushwa kufanya majukumu yake kwa umakini zaidi katika mechi iliyochezwa Januari 30, 2020 kwenye Uwanja wa Taifa. Aidha, Kamishina wa mchezo huo, Abdallah Zongo ameondolewa kwenye orodha ya Makamishina kwa kosa la kutoa taarifa yenye upungufu. Adhabu hiyo ni kwa kuzingatia Kanuni namba 40(1) kuhusu Udhibiti Kamishina.

 

LIGI DARAJA LA KWANZA: Mchezo wa Friend Rangers vs Dodoma FC, kiongozi wa Klabu ya Friends Rangers, Heri Chibakasa amepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kosa la kupigana na washabiki wa timu pinzani.

 

LIGI DARAJA LA PILI: Mechi ya Dar City dhidi ya African Sports, mwamuzi Salum Mkole amefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kuonyesha udhaifu katika usahihi wa kutoa kadi katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 31, 2020 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni namba 39(1) kuhusu Udhibiti wa Waamuzi katika mechi iliyochezwa Februari 01, 2020 kwenye Uwanja wa Karume, Dar. Vilevile katika mchezo huo mchezaji wa African Sports, Rajabu Kipango amepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kumpiga mchezaji wa timu pinzani.

Leave A Reply