The House of Favourite Newspapers

Rekodi Za Bocco vs Yanga Zinashtua

0

TIMU ya Simba, leo jioni itakuwa wageni wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mchezo huo ni wa pili kuzikutanisha timu hizo msimu huu baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 uliochezwa Januari 4, mwaka huu.

 

Matokeo hayo yalipokelewa kwa shingo upande na mashabiki wa Simba ambao wengi wao hawakufurahia, walikuwa na imani kubwa ya kuiona timu yao ikishinda mechi hiyo kutokana na ubora wa kikosi chao jinsi kilivyokuwa wakati huo ukilinganisha na kile cha Yanga.

 

Katika mchezo wa kwanza wengi waliipa nafasi kubwa Simba ya kushinda, lakini safari hii, hakuna ambaye ametoa nafasi kwa upande mmoja. Wengi wao wanasema kwa sasa mzani umebalansi kwani vikosi vyote vipo imara. Ukiacha na hilo, pia kuna mambo mengi ambayo yanatarajiwa kujitokeza uwanjani kutokana na ukubwa wa mechi hiyo jinsi ulivyo hapa nchini.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na rekodi mbambali ambazo baadhi ya wachezaji na makocha wataziweka ama kuzivunja zilizotangulia.

 

Nikuulize kitu, unaifahamu rekodi ambayo anaishikilia kwa sasa mshambuliaji na nahodha wa Simba, John Bocco dhidi ya Yanga tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Azam FC msimu wa 2017/18? Kama ulikuwa hufahamu, Spoti Xtra linakupatia rekodi hiyo ambayo inaweza kukushtua.

 

Licha ya Bocco kuwa miongoni mwa washambuliaji wakali hapa nchini kwa sasa huku akiwa anashikilia rekodi ya kufunga mabao zaidi ya 100 katika Ligi Kuu Bara tangu aanze kucheza, hana furaha akikutana na Yanga. Rekodi zinaonyesha kuwa tangu Bocco ajiunge na Simba msimu wa 2017/18 na timu hiyo kucheza mechi tano za ligi kuu dhidi ya Yanga, hajafunga bao lolote.

 

Hali hiyo imekuwa ikimkosesha raha kwani licha ya kupambana vilivyo uwanjani, lakini amekuwa hana bahati ya kuifunga Yanga ukilinganisha na wakati alipokuwa Azam FC. Katika mchezo wake wa kwanza akiwa na kikosi cha Simba msimu wa 2017/18 alipocheza dhidi ya Yanga Oktoba28, 2017, Bocco hakuweza kufanya lolote katika mechi hiyo ambayo matokeo yakiwa sare ya bao 1-1.

KATIKA MCHEZO HUO BAO LA SIMBA LILIFUNGWA NA SHIZA KICHUYA.

Katika mchezo wa marudiano msimu huo, mambo yalikuwa magumu kwa nyota huyo kwani hakufanya lolote licha ya timu yake ya Simba kushinda bao 1-0. Mchezo huo ulichezwa Aprili 29, 2018 na bao hilo lilifungwa na beki wa Simba, Erasto Nyoni. Katika msimu ya 2018/19, mambo pia yaliendelea kuwa magumu kwa Bocco.

 

Kwenye mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo, Septemba 30, 2018, matokeo yalikuwa ni 0-0. Mchezo wa marudiano ambao ulichezwa Februari 16, 2019, Simba ilifanikiwa kushinda bao 1-0, bao hilo pekee la Simba lilifungwa na Mnyarwanda, Medie Kagere.

 

Msimu huu pia katika mechi ya kwanza kuzikutanisha timu hizo, mambo pia hayakuwa sawa kwa Bocco, kwani katika mchezo huo hakuweza kufunga bao lolote. Matokeo katika mchezo huo yalikuwa ni 2-2 ambapo mabao ya Simba yalifungwa na Mkongomani, Deo Kanda na Kagere.

 

Siku hiyo Bocco alianzia benchi na kuingia uwanjani dakika ya 69 kuchukua nafasi ya Kagere. Kutokana na hali hiyo, unaweza kusema kuwa Bocco hana bahati ya Yanga tangu alipotua Simba akitokea Azam.

 

Hata hivyo, acha tusubiri katika mechi ya leo jioni tuone kama rekodi yake hiyo kwa Yanga itaendelea kuwa hivyo au ataivunja. Rekodi zinaonyesha kuwa, Bocco akiwa ni mchezaji wa Azam, alikuwa akifunga sana dhidi ya Yanga.

Leave A Reply