The House of Favourite Newspapers

Rich, Lulu wafanya kweli tuzo za African Magic

0

Na Saleh Ally, Lagos
HATIMAYE Bongo Movie imeng’ara baada ya Watanzania wawili kushinda tuzo mbili katika African Magic Viewers Choice Awards (AVCA).
Watanzania hao ni mkongwe Single Mtambalike ‘Rich Rich’ ambaye ameshinda Tuzo ya Filamu Bora Afrika Mashariki kupitia Filamu ya Kitendawili ambayo pia alikuwa anachuana na Mtanzania Amri Amri Shivji kupitia filamu ya Samaki Mchangani pamoja na Wakenya.
Elizabeth Michael ‘Lulu’ naye ameshinda tuzo ya Mtayarishaji wa Filamu Bora ya Afrika Mashariki akiwashinda Watanzania wengine, Honeymoon Mohammed na Stamford Kahore.
Katika sherehe za tuzo hizo zilizofanyika katika Hoteli ya Eko katika Kisiwa cha Victoria jijini Lagos, Nigeria, Waganda na Wakenya ndiyo waliopewa nafasi ya kuzitwaa.
Ushindi wa Rich na Lulu ni kama mwamko mpya wa tasnia ya filamu Tanzania ambayo ilionekana kuporomoka na kukosa umoja sahihi.
Wawili hao walionekana kuwa ni wenye furaha na Rich alisema ni furaha kubwa kwake inayozidi kifani.
“Nimeigiza kwa miaka 18 nikisubiri tuzo kubwa kama hii, lakini leo nimeonyesha unavyoweza kupambana bila ya kuchoka,” alisema Rich.
Kwa upande wa Lulu alisema: “Nimechanganyikiwa kabisa, kweli nimefurahi na shukrani kubwa kwa mashabiki kutokana na uamuzi wao wa kunisaidia na kunichagua.”

Leave A Reply