The House of Favourite Newspapers

Ripper Mcongo Wa Norway Awapa Mchongo Diamond, Ali Kiba

0

MWANAMUZIKI mahiri mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayefanya shughuli zake za muziki nchini Norway kwa lugha ya Kiswahili na Kingereza, Andrew Ripper ameonyesha nia ya kufanya kazi na wasanii wa hapa nchini Tanzania.

 

Ripper ambaye ni mkali wa kuimba na kucheza aina mbalimbali za muziki, kwa sasa anatamba na nyimbo za Dance Together na Jack & Rose ambazo zimeshika chati katika 10 Bora ya MTV Based Afrika pamoja na ile ya MTV Worldwide.

Mwanamuziki huyo ambaye alianza shughuli za muziki tangu akiwa mdogo hasa alipokuwa akiishi katika miji ya Kitwe na Lusaka nchini Zambia anasema kwa sasa ameanza kuona mwanga wa kazi zake za muziki.

 

Akizungumzia muziki wa Bongo, Ripper alisema amekuwa akifuatilia muziki wa hapa nchini kwa ukaribu akiwataja wasanii baadhi yao ni Ali Kiba, Mimi Mars, Ray Vanny, Harmonize, Barnaba Classic na Vanessa Mdee.

 

Alisema anatambua nafasi ya lugha ya Kiswahili katika muziki  ndiyo maana amekuwa akiitumia lugha hiyo huku akiwataka wasanii wa Tanzania kuwa tayari kufanya naye kazi za muziki.

 

Alisema kufanya kazi na wasanii wa hapa nchini itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwatangaza nchini Norway ambapo kuna fursa nyingi katika biashara ya muziki hasa matamasha.

Aliyataja matamasha makubwa ya muziki  aliyowahi kushiriki ambayo hata wasanii wa Tanzania wanaweza kuwatafutia nafasi ambayo ni Tamasha la Muziki la Oslo, Canal Street Kilden Street House ambalo ni

kati ya matamasha makubwa nchini Norway.

 

Aliongeza kuwa wasanii wengi wakubwa kama vile Wyclef Jean, Salif Keita, Timbuktu, Madcon na Philip Emilio wamewahi kushiriki.

 

Alisema kuwa mbali na kutaka kufanya kazi na wasanii wa hapa nchini pia angependa kufanya kazi na wasanii kama vile Tekno wa Nigeria na wengine mbalimbali wakubwa barani Afrika akiwamo Diamond Platinumz.

Kwa sasa ameshafanya kazi na wasanii kadhaa kutoka Zambia kama vile T Sean na T Bwoy.

 

Pia aliongeza kuwa angependa kufanya kazi na watayarishaji wa muziki kutoka Tanzania kisha baada ya hapo safari iendelee kwa kutangaza soko lake nchini Kenya na Uganda.

 

Alisema: “Ninapenda kufanya kazi na wasanii wa Tanzania kwa kuwa kwanza muziki wa Tanzania umekua na ni muziki ambao unavutia kusikilizwa, katika sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Afrika.

 

“Nimeamua kuimba kwa Kiswahili baadhi ya nyimbo na nitaendelea kukitangaza Kiswahili pia lakini ngoja Corona iishe hakika nitafika Tanzania kwa kazi zaidi,” alisema Ripper ambaye katika ukurasa wa Instagram anapatikana kwa jina la @Andrewripperofficial.

Leave A Reply