The House of Favourite Newspapers

Roma, Mr Blue na Darassa Kuliamsha Dude Idd Mosi Dar Live

0

 

Roma akiwa darasani anafundisha somo la hisabati.

BAADA ya kufanya miujiza katika bonge la shoo la Nichane Nikuchane lililofanyika katika Mkesha wa Mwaka Mpya 2016, mkali wa michano asiye na mpinzani Bongo, Ibrahim Musa ‘R.O.M.A Mkatoliki’ anatarajia kuliamsha dude jipya sikukuu hii (Idd Mosi) kwenye Ukumbi wa Dar Live uliopo MbagalaZakhem jijini Dar. Akizungumza na Championi Ijumaa, Mratibu na Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa,

mara ya mwisho kwa R.O.M.A kufanya shoo ilikuwa Dar Live na safari hii anarudi akiwa mpya ndani ya uwanja huo akiwa na sapraiz kibao katika shoo kabambe inayotambulika kama Nishushe Dar Live. “Tunajua kiu ya mashabiki wengi kumuona live R.O.M.A akikamua jukwaani na safari hii tena tumewaletea mtu wenu.

Ni wakati kwa shabiki yoyote mpenda burudani kujitokeza na kukata kiu kwa shoo ya kihistoria ambayo ataliamsha dude msilotegemea. “Kama mtakumbuka shoo yake hiyo ya Mkesha wa Mwaka Mpya alikuwa katika michano mikali na msanii Darassa na mliona shughuli yake.

Safari hii anashuka kuchukua kijiji chake na kuondoka nacho,” alisema Mbizo. Msikie R.O.M.A mwenyewe “Sijawahi kuwaangusha mashabiki wangu tangu nimeanza muziki. Siku zote ni mzee wa kuondoka na kijiji. Nitadondosha ngoma zangu zote kali kama Viva Roma Viva, K, Ivan, Kaa Tayari na nyingine kibao kikubwa njoo wewe na yule tujumuike pamoja na kumshuhudia R.O.M.A mpya nikiwa na ngoma mpya kwa mara ya kwanza tangu mwaka uanze,” alisema R.O.M.A.

Mr Blue yumo! Mbizo aliongezea kuwa mbali na uwepo wa R.O.M.A

siku hiyo jukwaa litapambwa na wakali wengine kibao wakiongozwa na Mr Blue na Darassa. “Wote tunamjua Blue anayebamba na nyimbo kibao kama vile Pesa, Mboga Saba na Baki Na Mimi. Mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia amshaamsha ambalo halijawahi kutokea popote,” alisema Mbizo.

Stamina wa michano Kuhusiana na mkali mwingine wa michano, Stamina, Mbizo alisema kuwa safari hii Dar Live imejiandaa kutoa burudani kwa mashabiki wake wote kwa kuangalia wanataka nini na kwa kipindi gani, hivyo katika sikukuu hiyo Stamina atawapa kinachostahili.

“Stamina ni mmoja kati ya wakali wa michano wabishi na kila wakitoa ngoma huwa gumzo. Alishawahi kufanya michano na R.O.M.A katika shoo moja lakini hii ya safari hii itakuwa zaidi ya chana nikuchane kila mmmoja akitambaa na biti la mwenzake,” aliongeza Mbizo.

Snura wa Chura Mbizo alimzungumzia pia mkali wa nyimbo za mduara, Snura a.k.a Mamaa Chura au Mamaa Majanga kuwa atakuwa miongoni mwa wakata kiu kwa mashabiki wote watakaojitokeza Dar Live. Alisema: “Chura zitakuwa za kumwaga na siku hiyo atakayepatia kucheza chura atapewa zawadi nono kutoka kwa Snura.

” Zanzibar Stars kuibuka Baada ya kupotea kwa muda, kundi kongwe la Muziki wa Mwambao, Zanzibar Stars litaibuka kwa mara ya kwanza ndani ya Dar Live likiwa na vichwa hatari kama Bi Mwanahawa, Sabaha Mchacho, Jokha Kassim, Mosi Suleiman, Ally Jay, Zubeda Mlamali  na wengine kibao.

Shoo ya watoto! Mbizo aliongeza kuwa, mbali na shoo hizo pia pazia la burudani litafunguliwa Sikukuu ya Idd Mosi mapema kuanzia saa 2:00 asubuhi kwa kundi la sarakasi lisilo na mpinzani Bongo, Wakali Dancers pamoja na Makhirikhiri kutoka Tanzania na mchekeshaji anayebamba katika Kundi la Ze Comedy, Bambo ambao wataliamsha kwa kutoa burudani kwa watoto.

Kutakuwa na michezo mingi ya watoto kama vile kubembea, kuteleza, kuogelea, kucheza ndani ya ndege na mingine mingi. Kiingilio Mbizo alimaliza kwa kutaja kiingilio kwa siku hiyo kuwa, burudani kwa wakubwa itakayoanza saa 2:00 za usiku itakwenda kwa shilingi 7,000 huku watoto ikiwa kiduchu cha shilingi 3,000 tu.

 

Leave A Reply