The House of Favourite Newspapers

Rostand Aanza Nyodo Yanga SC

    Youthe Rostand.

BAADA ya kuwaaminisha uwezo wake mashabiki wa Yanga, kipa wa timu hiyo, Youthe Rostand amesema anataka kuona Ligi Kuu Bara ikimalizika yeye akiwa kipa bora wa msimu huu.

Nafasi ya kipa bora wa ligi kuu inashikiliwa na kipa wa Simba, Aishi Manula ambaye alitwaa msimu uliopita akiwa na Azam FC.

 

Rostand raia wa Cameroon ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kuiwezesha Yanga kutinga 16 bora ya Kombe la FA baada ya kupangua penalti tatu dhidi ya Ihefu FC ya Mbeya.

Wachezaji wa Yanga wakiendelea na mazoezi.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Yanga na Ihefu zilitoka sare ya bao 1-1 lakini Wanajangwani wakashinda kwa penalti 4-3.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Rostand alisema anafanya bidii mazoezini kila siku huku akifuata maelekezo ya kocha wake, Juma Pondamali ili awe bora.

 

“Kila siku nataka niwe bora, kwa maana ya kuonyesha kiwango changu nikiwa golini nikiitumikia Yanga, hivi karibuni nilikuwa nikibezwa juu ya kiwango changu tunapofika kwenye penalti.

 

“Nilipambana mazoezini nikisema ipo siku uwezo wangu utaonekana, nashukuru hilo nimelimaliza na kikubwa ninataka kuona mwishoni mwa msimu ni kuwa kipa bora,” alisema Rostand.

Comments are closed.