The House of Favourite Newspapers

Sababu Sita Wanawake Kupata Ukimwi Zaidi ya Wanaume

ZIPO sababu sita ambazo zinasababisha wanawake wengi zaidi kuonekana wanapata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi ukilinganisha na wanaume. Sababu hizo ni kama zifuatazo;

  • MAUMBILE YA KIBAOLOJIA

Wanawake wapo katika hatari zaidi ya kupata Virusi Vya Ukimwi ukilinganisha na wanaume kwa kuwa maumbile ya mwanamke sehemu nyeti ni rahisi kupata michubuko wakati wa tendo la ndoa au kujamiiana hivyo kurahisisha virusi vya Ukimwi kupenya.

 

Aidha maumbile ya mwanamke hupokea mbegu za kiume kutoka kwa wanaume wakati wa tendo la ndoa, iwapo mwanamke atafanya mapenzi na mwanaume mwenye Virusi Vya Ukimwi, ni wazi anaweza kuambukizwa virusi vya Ukimwi.

  • TABIA NA MAZINGIRA HATARISHI

Tabia na mazingira hatarishi ambayo husababisha hatari zaidi kwa wanawake kuambukizwa Virusi vya Ukimwi ni pamoja na kufanya biashara ya ngono na kuanza mapenzi katika umri mdogo.

 

  • MFUMO DUME

Mfumo dume uliokuwepo katika jamii yetu unawapa fursa wanaume kuamua kufanya ngono na wanawake wengi hivyo kuwa rahisi kupata maambukizi ya Ukimwi.

 

  • KUTOTUMIA KINGA

Baadhi ya watu kutotumia kinga (kondom) wakati wa kujamiiana yaani kufanya ngono zembe kwa wapenzi wapya wakati hawajui afya zao huku wakiwa wanajua kuna janga la Ukimwi ni hatari.

 

  • WANAUME KUOA WASICHANA WADOGO

Baadhi ya wanaume wanaoa wasichana wenye umri mdogo kwa nguvu baada ya wazazi wao kupokea mahari jambo ambalo ni ukatili wa kijinsia.Mfumo huu unasababisha wanawake kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi na hata kushindwa kueleza ukweli kwa wenza wao kuhofia kuachika, kutengwa au kufukuzwa katika familia.

  • KUJITOKEZA KUPIMA

Wanawake wengi hujitokeza kupima kuliko wanaume hivyo nitoe rai kwa wanaume kujitokeza kupima wasitumie wenza wao kama kipimo cha maambukizi ya Ukimwi. Inakisiwa kuwa kwa Tanzania idadi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi imefikia milioni moja na laki tano huku idadi ya wanawake ikiwa kubwa zaidi kulinganisha na wanaume.

 

NJIA YA KUJIKINGA NA UKIMWI

Kwa siku za karibuni, kumekuwa na matokeo chanya kwenye mapambano na ugonjwa wa Ukimwi, sasa hivi watu wenye virusi vya Ukimwi wanaishi maisha yenye afya njema na kwa muda mrefu kwa msaada wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi (antiretroviral therapy (ART). Pia matumizi sahihi ya dawa hizi husaidia kupunguza muendelezo wa uambukizaji kwa wengine.

 

Kazi kubwa pia imefanyika ili kuzuia na hata kumaliza kabisa maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua. Ingawa kuna matokeo yote hayo chanya, lakini bado kuna sehemu kubwa ya jamii bado haina uelewa juu ya ugonjwa huu.

 

Virusi Vya Ukimwi vinaweza kuambukizwa kwa njia mbalimbali kama; kuambukizwa kwa mtoto mchanga wakati akiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa au kwa kunyonyeshwa na mama anayeishi na virusi vya ukimwi.

 

Hivyo, kabla na baada ya kuanza kubeba ujauzito, inashauriwa kupima afya na kuhudhuria vyema kliniki kwa ajili ya vipimo na ushauri juu na njia za kuondoa maambukizi haya. Wengine huambukizwa Ukimwi kwa kuwekewa damu yenye virusi vya ukimwi au kutumia vitu vyenye incha kali sindano, viwembe, nk. vilivyo na virusi vya ukimwi.

JINSI YA KUJIKINGA NA KUZUIA MAAMBUKIZI YA UKIMWI

Hakikisha unatumia kinga unapojamiiana na mtu ambaye hujuia afya yake. Pia nenda kapime na upate tiba ya magonjwa mengine ya zinaa kama unayo kwani kuwanayo fufanya uwezekano mkubwa wa kuambukizwa virusi vya Ukimwi.

 

Hakikisha damu unayowekewa hospitali imepimwa na haina virusi vya ukimwi, kwa wanaume tunashauri wasiotahiriwa watahiriwe ili kupunguza maambukizi.

 

USHAURI

Matumizi ya mapema na yaliyo bora ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) husaidia kuwafanya waathirika waishi maisha marefu na afya bora pia kupunguza maambukizi kwa wengine. Hivyo wahi kupima na ukigundulika umeathirika utaanzishiwa ARV’s.

Comments are closed.