The House of Favourite Newspapers

Sababu za Magufuli kutosafiri nje zajulikana

0

Stori: Elvan Stambuli, UWAZI

DAR ES SALAAM: Sababu kuu moja inayomfanya Rais John Pombe Peter Magufuli kutosafiri kwenda nje ya nchi, imejulikana.

Chanzo chetu cha habari cha kuaminika ndani ya serikali kimesema sababu kuu zinazomfanya kiongozi huyo wa nchi asisafiri nje ya nchi ni ‘uozo’ alioukuta ndani ya serikali na idara zake baada ya kushika madaraka hayo makubwa.

“Ukweli ni kwamba idara nyingi za serikali zilikuwa zimeoza kwa rushwa na kulikuwa na mianya mingi ya upoteaji wa fedha za serikali, hivyo rais akaamua ni vema azibe kwanza mianya hiyo na kuondoa uozo ndipo aanze safari za nje,” kilisema chanzo.

Kiliongeza kuwa, Idara ya Usalama wa Taifa ilimpa taarifa rais ya mambo mengi likiwemo suala la bandari zetu kubwa tatu nchini kuwa zinavujisha mapato ya serikali ndiyo maana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefanya ziara za ghafla Bandari ya Dar, Tanga na Mtwara na kugundua kuwa waliyoelezwa ni kweli.

Aidha, chanzo hicho kilisema pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitajwa na wana usalama wa taifa kuwa nako kulikuwa na uvujaji mkubwa wa mapato ya serikali na ndiyo maana viongozi wengi wa idara hiyo wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi lakini zoezi hilo limesaidia na sasa inakusanya zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi.

“Hali kwa sasa inaanza kuridhisha na inawezekana baada ya miezi mitatu, yaani ikifika Juni rais anaweza kuanza kwenda nje ya nchi,” kilimaliza.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga alisema moja ya sababu za rais kutotoka nje ya nchi ni ukata wa fedha alioukuta serikalini wakati akiingia madarakani na kupata muda wa kuendelea kuunda serikali yake.

 “Rais alikuta serikali iko katika hali ngumu sana kifedha, akaona utendaji kazi lazima asimamie mwenyewe. Kwa hiyo kote huko ambako alitakiwa kwenda kwa miezi sita ya kwanza aliomba radhi na ameeleweka kabisa na ninadhani kazi hii ya kuweka msingi, mwelekeo na msimamo itaendelea kwa miezi minne au mitatu,” alisema Balozi Mahiga na kukaririwa na vyombo vya habari.

 Alipoulizwa ni vitu gani ambavyo rais asipovisimamia vinaweza kuharibika, alisema: “Kwa mfano masuala ya usimamizi wa fedha, tumeona taasisi zinavyopambana, watu kupoteza ushahidi, komyuta zinaibiwa, mafaili yanaibiwa, kuna maamuzi mengine ni rais tu anaweza kutoa uamuzi.”

 Alisema kuna taasisi muhimu, mashirika ya umma yapo mengi na yanahitaji mabadiliko, hivyo rais ni lazima asimamie.

“Kwakweli rais wetu ana nguvu ya kipekee, kwa sababu kwa siku labda ana saa tatu tu za kulala usingizi,” aliongeza kusema.

Uwazi lilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Grayson Msigwa juzi kwa njia ya simu hakupatikana.

Leave A Reply