The House of Favourite Newspapers

Sadiki: Najifunza Mengi kwa Madiwani na Viongozi wa CCM Wilayani Muheza

0

 

Kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Muheza, Sadiki Rajabu amesema madiwani wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, ndiyo walimu wake wa masuala ya siasa na uongozi na kwamba mafanikio aliyonayo, yanatokana na ushauri na nasaha zao.

 

Ameongeza kuwa, pia amekuwa akijifunza mengi kwa viongozi wa CCM Wilaya ya Muheza kuanzia kwa Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya, Wenyeviti na Makatibu wa Jumuiya za CCM Wilaya, Wenyeviti na Makatibu wa CCM na Jumuiya zake ngazi ya Kata na Matawi.

 

Hamisi Sadiki Rajabu amesema hayo mapema leo Alhamisi tarehe 02/02/2023 wakati alipohudhuria kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani Muheza kilichohusu kupitisha Mpango wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.

 

“Ili uweze kufanikiwa katika masuala ya siasa na uongozi huwezi kuacha pembeni Waheshimiwa Madiwani pamoja na Viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya, Kata na Matawi. Viongozi hawa wamejioambanua katika siasa yenye kuleta tija hasa katika kuinua maisha ya wana Muheza.”

 

Hamisi ambaye kwa nyakati tofauti aligombea Ubunge katika Jimbo la Muheza pamoja na Ubunge wa Afrika Mashariki ameeleza zaidi kuwa, Viongozi hawa wamemuweka katika ramani ya siasa na uongozi kutokana na kujifunza kutoka kwao na nasaha za mara kwa mara.

 

Kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia Mkuu wa Wilaya mpya wa Wilaya hiyo Mhe Saidi Irando, kilishuhudia mjadala mkubwa wa bajeti hiyo ambayo imeonesha mwanga wa maendeleo katika Wilaya hiyo kwa mwaka ujao. Sambamba na hilo, Madiwani walipata nafasi ya kujadili Mpango huo kwa kuonesha namna wanavyotaka Muheza iwe.

 

Hamisi ametoa rai kwa Wananchi kupenda kuhudhuria vikao hivyo ili kupata taarifa sahihi na kujua mustakabali wa maendeleo ya maeneo yao wanayoishi.

Leave A Reply