The House of Favourite Newspapers

Safari ya Taifa Stars Afcon 2023 Kuanza Leo

0

Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) hufanyika kila baada ya miaka miwili na kwa sasa ushirikisha jumla ya timu za taifa 24 ambazo hugawanywa katika makundi sita

 

Taifa Stars leo itafahamu washindani wake katika mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Afcon 2023 zitakazofanyika huko Ivory Coast.

 

Droo ya mashindano hayo ya kufuzu Afcon 2023 itachezeshwa leo huko Douala, Cameroon kuanzia saa 12:30 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki na itaendeshwa na nyota wawili wa zamani wa soka Rigobert Song na Emmanuel Amunike.

 

Rigobert Song ni mshindi wa taji la Afcon mara mbili akiwa na kikosi cha Cameroon akifanya hivyo mwaka 2000 na 2002 wakati Amunike alishinda taji hilo akiwa na kikosi cha Nigeria mwaka 1994.

 

Katika droo hiyo jumla ya timu 12 ambazo ziko chini katika viwango vya ubora wa soka kati ya 54 barani Afrika ambazo ni wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), zitaanzia hatua ya awali kwa kucheza mechi za mtoano kupata timu sita (6) ambazo zitaungana na nyingine 42 kupata jumla ya timu 48 zitakazogawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja.

 

Timu hizo 12 ambazo zitalazimika kuanzia hatua ya awali ni Lesotho, Eswatini, Botswana, Gambia, Sudan Kusini, Mauritius, Chad, Sao Tome & Principe, Djibouti, Somalia, Shelisheli na Eritrea.

 

Baada ya hapo, timu mbili zitakazoongoza kila kundi, zitafuzu fainali hizo zitakazofanyika Ivory Coast kuanzia Juni 23 hadi Julai 23 mwakani.

 

Taifa Stars itakuwa inatafuta tiketi ya kushirki fainali za Afcon kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 zilipofanyika Nigeria na mwaka 2019 zilipoandaliwa huko Misri.

Leave A Reply