The House of Favourite Newspapers

Sakata la Kitita Kipya NHIF, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Atoa Onyo

0

 

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

SERIKALI imesema haitamvumilia Mtoa Huduma yeyote ambaye atakiuka sheria ya kutoa huduma hususan wakati huu wa utekelezaji wa Kitita kipya cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Lindi ambapo aliwaagiza Watoa huduma hao kuzingatia Mkataba wao na kuwahudumia wanachama ikiwamo kuheshimu maadili yao kama Madaktari.

“Nimeona habari na matangazo yakisema watawatoa Wagonjwa waliopo wodini ndani ya masaa 48 nataka kusema ni marufuku kuondoa Wagonjwa waliopo wodini kwasababu kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya Madakatari na katika hili hatutamvulia mtoa huduma yeyote,” alisema.

Aidha alitumia nafasi hiyo kuzielekeza Hospitali zote za Serikali kujiandaa na kuweka utaratibu mzuri wa kupokea Wagonjwa wengi zaidi watakaoshindwa kupata huduma kwenye Vituo binafsi na kuwahudumia.

“Kila Mtoa Huduma za Afya kwa wanachama wa NHIF ameingia mkataba na NHIF, hivyo wazingatie masharti ya mikataba waliyoingia na NHIF katika kuwahudumia wanachama wake,” alisema Waziri akiwa ziarani Mkoani Lindi.

Alitoa rai kwa hospitali zote binafsi zilizositisha kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kuendelea kutoa huduma na kutekeleza kitita kipya.

“Kamati ya Kitaalam niliyoiunda iendelee kufanya majadiliano na watoa huduma wakati kitita kikiendelea kutumika na wanachama wakiendelea kupata huduma,” alisema na kuongeza.

“Nazielekeza hospitali au vituo vyote binafsi na vya umma kuendelea kuwapokea wagonjwa wa dharura pindi wanapofika katika vituo vyao kwani hili ni takwa la kisheria namba 151 la usajili wa vituo binafsi vya afya na kanuni yake namba 32, kutokuwapokea wagonjwa wa dharura ni kuvunja sheria”. Alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa kusimamia maelekezo ya Serikali katika kuwapatia wananchi na wanachama wa NHIF huduma.

Leave A Reply