The House of Favourite Newspapers

Samatta ashinda kiatu Ubelgiji, baba amchinjia jogoo

MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta ameweka rekodi mpya nchini Ubelgiji baada ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mwenye asili ya Afrika ‘Ebony Shoe’ huku baba yake mzazi akitoa ahadi ya kumchinjia jogoo leo.

 

Samatta anayekipiga katika klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji ‘Jupile pro Ligue’, ameshinda tuzo hiyo kutokana na mchango wake kwenye timu yake inayoongoza ligi hiyo huku akiongoza katika orodha ya wafungaji akiwa na mabao 20.

Nahodha huyo wa Taifa Stars ameweka rekodi mpya ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo na wa pili kwa Afrika Mashariki baada ya Mohammed Tchité kutoka Burundi kushinda mwaka 2007 akiwa na klabu ya Anderlecht.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Baba mzazi wa mshambuliaji huyo, mzee Ally Samatta alisema kuwa kwa upande wake amefurahishwa na tuzo hiyo huku akitoa ahadi ya kuchinja jogoo kusherekea ushindi huo.

 

“Kiukweli nina furaha kubwa kutokana na kijana wangu kushinda tuzo hiyo na hii imetokana na yale ambayo tumekuwa tukimueleza wakati wote juu ya kuongeza juhudi, nia nidhamu na upendo katika kazi yake.

 

“Furaha yangu haielezeki kwa kile ambacho amekifanya kwa sababu hata ubingwa wa ligi wana asilimia kubwa ya kubeba msimu huu, furaha yangu sitaki ipite kimyakimya kesho (Jumatano) nitamchinjia jogoo kubwa kusherekea kama nilivyofanya wakati ule alipoingia kwenye kikosi bora cha Europa,” alisema mzee Samatta.

Comments are closed.