The House of Favourite Newspapers

Sare vs Namungo Fc, Yanga Sc Inawalazimu Kucheza Mechi Mbili Pamoja

0

KIKOSI cha Yanga kwa sasa kiko katika nafasi ya pili ya Ligi Kuu Bara baada ya mechi 11 za Ligi Kuu Bara. Yanga imeshinda mechi saba, sare nne na ndiyo timu pekee ya Ligi Kuu Bara haijapoteza mechi hata moja hadi sasa.

Katika mechi hizo 11, Yanga imefunga mabao 13 na kuruhusu mabao manne tu. Hivyo kuifanya kuwa timu iliyofunga mabao machache zaidi katika ‘Top Three’ lakini iliyoruhusu mabao machache zaidi katika ligi hiyo hadi sasa.

 

Unaona tayari Yanga imeingia katika presha ambayo itapungua sana kama Yanga itafanikiwa kuishinda Azam FC mechi ya leo Jumatano.

 

Kama haitakuwa hivyo, maana yake, sare itaifanya Simba ipande kileleni ikiwa na pointi 26 lakini ina mabao mengi ya kufunga yanayotengeneza wastani mzuri kwa maana ya GD.

 

Presha inakuwa kubwa kwa kuwa unaona Yanga ilikuwa ina tofauti ya pointi sita dhidi ya Simba, lakini sasa ni pointi mbili tu ambazo zinatengeneza presha wakati Yanga inakwenda kukutana na Azam FC ambayo wanalingana nayo pointi.

Hili si jambo dogo kwa Yanga na inaonyesha wazi wanapaswa kujipanga hasa kwa kuwa kama ni sare dhidi ya Azam FC, halafu Simba wakashinda watalingana pointi na Simba watakwenda kileleni kwa mabao yao.

 

Ikiwa Yanga itapoteza, maana yake Azam FC itakwenda kileleni na Simba watapaa juu ya Yanga kama watashinda dhidi ya timu ijayo baada ya kumaliza mechi ya kimataifa wikiendi hii inayokuja na Yanga watashuka nafasi ya tatu.

 

Kinachopaswa kuiondolea Yanga presha kubwa ili iweze kusonga mbele ni ushindi dhidi ya Azam FC ili ipae kileleni ikiwa na 28, maana yake kama Simba itashinda, itakuwa na pointi 26, mbili chini ya Yanga.

Kushinda dhidi ya Azam FC, haitakuwa mechi nyepesi kwa kuwa Azam FC wanajua nafasi yao ya kubaki kileleni ni kuishinda Yanga na si vinginevyo.

 

Azam FC wanajua sare au kupoteza ni kuondoka kileleni na kujitengenezea ugumu wa kiwango cha juu sana na sasa hali inaonyesha mwendo wa Simba unazifanya Yanga na Azam FC kuwa katika presha lkubwa.

Kunapokuwa na mtu anakukimbiza, presha inakuwa kubwa kuliko yule ambaye anayemkimbiza mwingine. Hii hali ndiyo wanayo Yanga na Azam FC kwa kipindi hiki.

 

Mechi dhidi ya Namungo FC ambayo Yanga walipata sare ya bao 1-1, ndiyo iliyoanzisha presha hii kwa kiwango cha juu. Maana kama Yanga ingeshinda, basi ingekuwa na pointi 27 ambazo zingeipeleka kileleni na Simba wasingeifikia hata kama ingepoteza dhidi ya Azam FC.

 

Presha imekuwa kubwa zaidi baada ya kudondosha pointi mbili wakati ikipata sare hiyo dhidi ya Namungo FC. Tena inaonyesha hivi, Yanga wanalazimika kushukuru angalau sare kwa kuwa wangeweza kuupoteza mchezo huo katika dakika za mwisho baada ya Namungo FC kupata penalti dakika za majeruhi.

 

Kinachotakiwa kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze kuutumia muda wake mwingi kuzungumza na wachezaji wake kuwaelezea umuhimu wa ushindi.

 

Kutumia muda mwingi kuwasoma Azam FC na kujua nini sahihi cha kufanya kabla na wakati wa mchezo huo lakini namba moja hata kama watakuwa wamejiandaa vipi ni kuikataa presha.

Kama Yanga watairuhusu presha, maana yake nafasi ya kupoteza mechi hiyo dhidi ya Azam FC itakuwa kubwa maana watashindwa kucheza katika kiwango chao.

 

Nasema hivi kwa kuwa kiuhalisia, bado kiwango cha Yanga hakijaimarika, hivyo kama ambavyo wengi wanazungumza kishabiki. Kama kunakuwa na presha wanaweza wakatengeneza nafasi kubwa ya kupoteza.

 

Wachezaji wakigundua umuhimu wa kuifunga Azam FC, halafu wakajiandaa na kujiamini na wacheze mpira wanaoumini basi wana nafasi ya kufanya vizuri.

Ambacho anapaswa kukikumbuka Kaze ni kwamba Yanga wataingia uwanjani kucheza mechi mbili kwa wakati mmoja wakati wakiivaa Azam FC.

 

Kwanza ni wao dhidi ya Azam FC, pili dhidi ya Simba. Dhidi ya Azam FC kwa kuwa ndiyo mechi wanayocheza uwanjani lakini watakuwa wakiwawazia Simba kwa mambo mawili, kwamba wakitoka sare au kupoteza na Simba akashinda atapanda juu yao, watalazimika kuiwaza na kuicheza ‘game’ ya Simba kwa kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili Simba wasipae juu yao, jambo ambalo lina presha kubwa sana.

SALEH ALLY

Leave A Reply