The House of Favourite Newspapers

Sasa Hali Inatisha… Mawazo Yanaua Mamilioni ya Watu

0

‘USICHUKULIE POA… msongo wa mawazo unaua’. Hiyo ni kauli ya watalaam baada ya kubainika kuwa mtu mmoja kati ya watano anakabiliwa na msongo wa mawazo ambao unaweza kumsababishia magonjwa hatari katika maisha yake. UWAZI linachambua.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2019 ya Taasisi ya kimataifa ya utafiti na uchambuzi wa masuala mbalimbali (Gallup Global Emotions Report), zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye umri kuanzia miaka 18 kuendelea wanakabiliana na tatizo la msongo wa mawazo.

MSONGO WA MAWAZO NI NINI?

Dk. Sadick Sizya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema msongo wa mawazo ni hali ya kuwa na mawazo mengi, ambayo mara nyingi mtu hushindwa kuyapatia ufafanuzi, ufumbuzi au mwafaka. Hali hii hutokea pale mtu anaposumbuliwa na jambo fulani katika maisha yake. Dk. Sizya anaongeza kuwa kuna madhara makubwa yanayotokana na hali ya msongo wa mawazo ambayo wakati mwingine husababisha mtu kupoteza uhai.

MADHARA YA MSONGO WA MAWAZO

Akifafanua kwa kina Dk. Sizya alisema moja ya madhara makubwa ya msongo wa mawazo ni kujiua, kupata matatizo ya moyo, ugonjwa wa kisukari, vidonda vya tumbo, shinikizo la juu au la chini la damu, kupatwa na kiharusi pamoja na magonjwa mengine yanayojitokeza kutokana na athari za msongo wa mawazo.

TATIZO LA MOYO

Dk. Sizya alisema licha ya kuwa ni dhana pana, lakini magonjwa ya moyo ndio yanayoongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani ambapo watu milioni 1.7 kila mwaka hufariki kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2017 ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema mtu anapopatwa na msongo wa mawazo hubadilika kitabia, kuna wengine hukosa hamu ya kula wakati wengine hupenda kula kupita kiasi, ambapo mwisho wa siku hupatwa na uzito kupindukia, presha na hata kisukari. “Lakini pia msongo wa mawazo hupandisha baadhi ya homoni ambazo husababisha mapigo ya moyo kwenda kwa kasi.

Sasa mapigo ya moyo yakienda kasi hayatokuwa na tija kwenye mwili wa binadamu kwa sababu badala ya kusukuma damu kwa mfumo wa kawaida, moyo hubaki kudunda tu kama ku-dance bila kusukuma damu kwa mtiririko sahihi.

“Damu isipofika kwa usahihi hususani kwenye ubongo ambao ndicho chakula chake, mtu hujikuta anapatwa na maumivu makali ya kichwa, kizunguzungu, kiharusi au kufariki ghafla kutokana na mshtuko wa moyo.

KUJIUA

Mtaalam wa masuala ya saikolojia kutoka Chuo kikuu cha Dalhousie kutoka Canada, Dk. Patricia Celan katika ripoti yake ya masuala ya kisaikolojia aliyoiwasilisha mwaka huu, amebainisha kuwa msongo wa mawazo hauwezi kuua, ila ndio chanzo cha magonjwa yanayoua kwa kasi duniani ikiwamo matukio ya watu kujiua.

Takwimu zilizotolewa mwaka jana na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kila mwaka watu 800,000 hupoteza maisha kwa kujiua ambapo kati ya watu 100,000 watu 12 hujitoa uhai.

Kutokana na msongo wa mawazo, kila sekunde 40 mtu mmoja hupoteza maisha kwa kujiua, kwamba kwa kila saa moja watu 90 hujiua duniani kote.

MAGONJWA YA AKILI

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Akili Muhimbili –Mloganzila, Dk. Fileuka Ngakongwa Oktoba mwaka huu, takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zimeonesha ongezeko la idadi ya wagonjwa wa afya ya akili hadi asilimia 10.8.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa kwa mwaka 2018/2019 idadi ya wagonjwa wa akili ilikuwa ni 29,166 huku mwaka 2019/2020 idadi ikipanda na kufikia 32,307.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania, Isaack Lema aliongeza kwamba msongo wa mawazo umesababisha ugonjwa wa akili kukua zaidi hususani kwa upande wa wanaume.

Alisema takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mwaka 2018/19, zimeonesha kuwa idadi ya wanaume wanaougua ugonjwa wa akili ni 18,535 huku wanawake wakiwa ni 10,631.

Alisema sababu ya idadi kubwa ya wanaume kukumbwa na magonjwa ya akili kuliko wanawake inatokana na tabia ya kutokuzungumza au kulia pindi wanapokumbana na matatizo.

DALILI ZA MSONGO WA MAWAZO

Akifafanua kwa kina kuhusu dalili za msongo wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam udara ya Saikolojia, Dk. Chris Mauki alianza kufafanua kuwa; “Wakati kila mmoja wetu akijitahidi kusukumana na kukimbizana na maisha ya kila siku, jitihada mbalimbali zinahitajika kukwepa msongo wa mawazo au wengine wanaita “stress” ambao huweza kusababisha athari katika afya na hisia zetu.

“Ni muhimu sana kila mmoja wetu akafahamu namna au mbinu za kuushinda msongo huu wa mawazo kabla haujakuzidi na kuleta athari mbaya zaidi katika maisha,” alisema.

Aidha, alisema dalili za madhara ya msongo wa mawazo kuwa ni maumivu ya mara kwa mara ya kichwa, matatizo katika usagwaji wa chakula “digestive problems”, maumivu ya kifua, matatizo ya kukosa usingizi na kuyumba kwa shinikizo la damu.

“Kuongezeka kwa msongo wa mawazo kunaweza kuongeza kiwango na mateso kwenye baadhi ya magonjwa aliyonayo mtu.

Matatizo kama vile shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, pumu, kisukari, sonona, magonjwa yanayohusiana na hofu, matatizo yanayohusiana na hisia, pamoja na matatizo au magonjwa ya ngozi huweza kuzidishwa kama mgonjwa ana kiwango kikubwa cha msongo wa mawazo,” alisema.

Aliongeza kuwa athari nyingine za msongo wa mawazo ni kinga kupungua mwilini, kuzeeka katika umri mdogo na matatizo ya kupoteza kumbukumbu.

“Kwa sababu ya kusumbuliwa na msongo wa mawazo, wako wengine hujitumbukiza kwenye ulevi wa pombe, uvutaji mkubwa wa sigara na dawa za kulevya, lakini jitihada zote hizi za kupunguza “stress” huwa na athari mbaya zaidi kiafya. Hapa najaribu kukusaidia kuziona njia bora na rahisi za kukabiliana na msongo wa mawazo kiufanisi na ukizingatia kuiboresha afya yako,” alisema.

MAMBO YA KUZINGATIA

“Jifunze kusema hapana. Kwa kuamua kukubali kufanya kila kitu kinachokujia mbele yako, kukubali kila mwaliko ulio mbele yako, kukubali kuongea na kila mtu anayetaka kukuona au kukutana na wewe au pia kuamua kufanya vitu tele visivyoongeza thamani kwako kunaweza kukufanya uhisi kuchoka, kuzidiwa na kuwa mwenye msongo wa mawazo.

“Ukweli ni kwamba watu wenye ufanisi, watu wenye furaha na watu wenye maisha yenye uwiano katika yale wanayoyafanya hujizuia sana kuhusiana na muda wao na hujiwekea mipaka katika maisha yao, kwa hiyo kujifunza kusema hapana kutakusaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuweza kuishi kwa ufanisi mkubwa katika maisha yako binafsi ya kila siku.

“Jaribu kufahamu udhaifu wako au yale usiyoyaweza, jifunze kujiwekea vipaumbele, jifahamu na jitambue, kuwa mwenye msimamo katika unachokitaka na usichokitaka na jiruhusu kuweza kusema “hapana” katika baadhi ya mambo.

Hakika mwili na nafsi yako vitakushukuru sana kwa hilo. “Jaribu kuvuta pumzi kwa kina. Mara nyingi mtu anapokuwa na msongo wa mawazo hupumua harakaharaka na kwa pumzi fupi kwa ajili ya vile mwili wake unavyokabiliana na msongo huo “fight or flight response”.

Hali hii inaweza kusumbua uwiano wa gesi ya mwili na kuongeza vipindi vya hofu na mshtuko, lakini hata hivyo kwa kupumua pumzi kubwa, ndefu na ya kina “breathing deeply” kunaweza kuwezesha mwili wako kupoa, kwasababu mtu anapopoa na kuondokana na hofu kule kupumua haraka haraka hutulia.

“Kwa kuamua kutumia mbinu hii ya kupumua pumzi ndefu na ya kina, unaweza kuituliza mishipa yako na kuusaidia mwili wako kukabiliana na msongo wa mawazo. Jaribu kukaa katika mkao mzuri, nyanyua mabega yako ili kupanua kifua chako, weka mkono wako mmoja katika kifua chako na mwingine kwenye tumbo.

“Kwa kufanya hivyo utaweza kuona jinsi maeneo haya yanavyoingia ndani na kutoka nje kadiri unavyopumua. Wakati unapumua, vuta pumzi ndefu na kuitoa taratibu kutumia pua zako na uruhusu lile shinikizo la mawazo ya msongo kutoka kila unapotoa pumzi nje. “Taratibu utaona kifua na tumbo vinapoa na kuanza kutulia.

Baada ya kuiona tofauti katika kufanya haya, basi endelea kuifurahia hali ya burudiko la nafsi mwili na moyo kwa muda kama wa dakika 10 au 20 kabla haujaendelea na mambo mengine,”alisema mtaalamu huyo wa saikolojia.

Leave A Reply