The House of Favourite Newspapers

Sekta Ya Mawasiliano Imefungua Fursa Mpya Ya Maendeleo Endelevu -Waziri Mohamed

0
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Serikali Mapinduzi Zanzibar Khalid Salum Mohamed akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Serikali Mapinduzi Zanzibar Khalid Salum Mohamed miaka ya hivi karibuni kumekuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya mawasiliano hapa nchini. Jamii kubwa ya watanzania mijini na vijijini imefikiwa na huduma za mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti.

Waziri Mohamed  ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Tehama yaliyofanyika mjini Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Bakari kwenye maadhimisho hayo.

Amesema  TCRA imeshiriki kikamilifu katika kufanya utafiti kwa ajili ya ujenzi wa minara 45 ya Mawasiliano ya simu kwenye maeneo mbalimbali hapa Zanzibar ambayo yalikuwa yakipokea huduma hafifu za Mawasiliano na baadhi ya maeneo hayakuwa na huduma kabisa na minara yote inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Nimearifiwa pia kuwa, hadi mwezi Machi 2023, idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka hadi kufikia watu milioni 33, na idadi ya watumiaji laini za simu kufika milioni 61.

Washindi wa kwanza wakipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Serikali Mapinduzi Zanzibar Khalid Salum Mohamed.

Hii inaonesha kwamba Tanzania ni nchi ambayo watu wake wanaweza kupata huduma mbalimbali za mawasiliano kwa gharama nafuu ikilinganishwa na nchi nyingine duniani na kuongeza upatikanaji na unafuu wa huduma mbalimbali za mawasiliano nchini ni uthibitisho tosha kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimejipanga vilivyo kuandaa mazingira bora na wezeshi kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa kidijitali” amesema Mohamed.

Amesema mazingira ya uboreshaji wa  mawasiliano yamesaidia utoaji wa huduma za kijamii, kufikia watu wengi zaidi katika maeneo ya mijini na vijijini, kuzalisha ajira, kuongeza pato la taifa, kufungua fursa mpya za maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii nchini na hivyo kuboresha maisha ya wananchi” amesema Mohamed.

Baadhi ya wanafunzi wasichana katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Mjini Zanzibar.

Amesema  Serikali ya Tanzania na SMZ zimekuwa zikifanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wake wanapata ujuzi wa kutumia teknolojia za kidigitali kwa lengo la kuwaendeleza kiuchumi, kielimu na kijamii. Mitaala ya vyuo vikuu, shule za sekondari na msingi imeboreshwa kuwezesha ufundishaji wa masomo ya TEHAMA yanayokwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kumwezesha mwanafunzi kutumia teknolojia hizo kufanya ubunifu wa kutatua changamoto za kijamii.

Amesema  TCRA kwa jitihada zao katika kuelimisha jamii, hususani vijana na kipekee wasichana na wanawake kuwawezesha  kupenda na kujifunza masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati kutokana umuhimu wa hayo masomo.

Amesema wasichana wanahitaji kuungwa mkono katika kujifunza masomo ikiwa  TCRA kwa kuwezesha na kuhamasisha wasichana katika kufikia ndoto zao.

Mohamed amesema TCRA imeanzisha vilabu vya kidigitali  katika vyuo na shule kwa lengo la kukuza ujuzi wa kigiditali (digital skills) na kuwezesha vijana kupata elimu bora juu ya matumizi salama ya teknolojia za kidigitali. Hatua hii inalenga kuwasaidia vijana kujenga ujuzi wao wa kiteknolojia na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya jamii zao kwa kufanya ubunifu mbalimbali.

Aidha amesema   TCRA imeanzisha vilabu hivi hapa Zanzibar vilivyopo Unguja na Pemba kwani ni hatua kubwa na muhimu katika kuendeleza TEHAMA na kukuza ujuzi wa TEHAMA kwa vijana.

Pia amepongeza kufanyika kwa  mafunzo kwa ajili ya wasichana yamefanyika kwa mafanikio hapa Zanzibar. Nimeelezwa kuwa jumla ya wasichana 80 wamepata mafunzo haya; 30 katika kituo cha Unguja na 50 katika vituo viwili vya Pemba. Hii ni hatua muhimu katika kuwawezesha wasichana na kuwapa nafasi sawa na wavulana katika ujifunzaji wa TEHAMA.

Amewataka  wakuu wa vyuo na shule za Sekondari hapa Zanzibar kuhakikisha kuwa kila chuo na Skuli ya Sekondari inakuwa na Klabu ya Kidijitali ili kuwahamasisha vijana wetu kupata ujuzi wa TEHAMA, ambao utasaidia kuleta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii.

Ujuzi huu ni muhimu sana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii yetu. Kama mnavyoona katika mawasilisho yaliyotolewa hapa, teknolojia ina jukumu muhimu katika kuboresha maisha yetu. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa shule na vyuo kutoa fursa hizi kwa wanafunzi wao ili waweze kuwa na ujuzi wa kutosha wa TEHAMA na kuchangia katika kuleta maendeleo ya jamii yetu.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Bakari amesema Siku ya Wasichana na TEHAMA Duniani, huadhimishwa kila mwaka  imetokana na makubaliano ya nchi wanachama wa Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU), ambapo TCRA ni mwakilishi wa Tanzania katika shirika hilo.

Amesema kuwa TCRA kwa kushirikiana na wadau wa elimu yaani (TAMISEMI, Wizara ya Elimu, TCU na NACTVET) kwa sasa wanaandaa Mwongozo utakaoelezea bayana namna ya kuanzisha na kuendeleza klabu za kidijitali katika shule za msingi, sekondari na vyuo.

TCRA inaamini kuwa kupitia klabu za Kidijitali katika kuongeza wabunifu wenye umri mdogo, wataalamu katika sekta ya Mawasiliano, ambayo ni sekta wezeshi;

-Kutoa elimu endelevu kwa wadau waliopo katika shule

-Kurahisisha mawasiliano pale panapokuwa na pengo la uelewa 

Dkt. Bakari amesema klabu za wanafunzi zinatumika kwenye kufikisha ujumbe wa kuhakiki laini za simu na kuwezesha wahusika kupata uelewa wa sekta ndogo tatu za mawasiliano.

Amesema wanathamini mchango  sekta ya Mawasiliano katika maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii kuona wasichana katika Taifa letu wanapata fursa ya kujifunza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupata wataalamu watakaolisaidia Taifa  kupiga hatua zaidi katika maendeleo hasa ukuzaji wa uchumi wa Kidijiti na uchumi wa buluu.

Dkt. Jabiri amesema kuwa Kauli mbiu ya siku ya Wasichana na TEHAMA duniani kwa mwaka huu inasema  “Ujuzi wa Kidijiti kwa Maisha”lengo la kauli mbiu hii ni kuhamasisha mafunzo na ujuzi wa Kidijiti kwa wasichana na wanawake ili kuongeza ubunifu katika sekta ya TEHAMA kama tunavyofahamu kuwa msingi wa maendeleo katika jambo lolote ni kupata mafunzo sahihi na kutumia taaluma hiyo kwa manufaa yako binafsi na jamii kwa ujumla.

Aidha amesema TCRA huadhimisha siku hii kila mwaka kwa kuandaa matukio mbalimbali ambayo ni  semina, midahalo kwa wasichana wa shule nchini kuhusu masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii na TEHAMA kwa ujumla.

Amesema TCRA iligawa vifaa vya TEHAMA (kompyuta) kwa shule 15 za wasichana Tanzania bara na visiwani, kwa lengo la kuhamasisha wasichana kujifunza masomo ya TEHAMA ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za ukuaji wa sekta. Aidha, kila mwaka, Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) hutoa kauli mbiu maalum inayohusu TEHAMA na mchango wake katika maendeleo ya jamii kwa ajili ya kuadhimisha maadhimisho hayo.

Amesema kwa  kuzingatia Kauli Mbiu ya mwaka huu, “Ujuzi wa Kidijiti kwa Maisha”, ni muhimu kuelewa kwamba ujuzi huu unaweza kuwa na athari chanya katika maisha yetu, hata kama unaanza kupata ujuzi huu kwa kiwango kidogo.

Amesema  TCRA imeratibu mafunzo ya muda mfupi ya TEHAMA kwa wanafunzi wasichana wa vyuo vikuu kupitia vilabu vya Kidijiti vilivyopo katika Mikoa ya Unguja na Pemba, Morogoro, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, na Mwanza.

Mafunzo haya yanajenga uwezo, ubunifu na ujuzi kwa wasichana katika kuandaa Programu Tumizi zitakazotatua changamoto katika jamii, pamoja na kuwapa fursa ya kujifunza ubunifu zaidi. Katika kipindi cha mafunzo ya siku nne, wanafunzi walipewa jukumu la kutambua tatizo la kijamii, kulichambua, na kupanga jinsi ya kutumia TEHAMA kutatua changamoto husika.

Hata hivyo amesema mafunzo yalijumuisha  kutengeneza muundo wa mfumo  kuandaa namna ya kuutekeleza kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu kutengeneza programu ya rununu), na hatimaye kuandaa mfumo wenyewe.

Amesema Wanafunzi waligawanywa katika vikundi tisa na walishindanishwa kulingana na ufanisi wa mipango yao na kuweka vigezo vya mchujo viliandaliwa, na siku ya mwisho ya mafunzo, wanafunzi walipata fursa ya kuwasilisha na kuelezea kazi zao kwa waratibu na walimu wa programu hii. Kikundi kimoja kilichofanya vizuri zaidi kilitambuliwa kupitia vigezo vya mchujo na kushindanishwa na washindi kutoka vilabu vingine nchini. Hatimaye, vikundi vitatu vilivyofanya vizuri zaidi vilichaguliwa.

“Tunatambua na kuthamini mchango wenu katika kufanikisha kazi hii, tunawaasa muendelee kuwaendeleza vijana hasa wasichana, kwa kuwajengea uwezo kwenye masomo ya STEM kwa ujumla na kwa upande wa TEHAMA muendelee kusisitiza matumizi salama ya TEHAMA ” Amesema Dkt.Bakari.

Amesema wanatarajia kwamba mtakuwa chachu kuwahamasisha wenzenu kupenda masomo ya Sayansi ili kuongeza ujuzi wa Kidijiti na pia kujiunga na vilabu vya Kidijiti katika vyuo na shule zenu.

Leave A Reply