The House of Favourite Newspapers

Senzo: Sikuwa na Furaha Simba, Luis Ana Mkataba Simba

0

ALIYEKUWA Mtendaji Mkuu Simba, Senzo Mazingisa Mbatha,  Agosti 20, 2020,  amewataka mashabiki wa timu hiyo ya Simba kukubaliana na kile ambacho kimetokea kwa sababu pamoja na yote mpira kwake ni kazi na unaendesha maisha yake.

 

Mazingisa alisema hayo kutokana na kufahamu kwake kwamba kwa namna moja au nyingine kuachana kwake na Simba huku akijiunga na Yanga ni maamuzi ambayo yamewaumiza mashabiki wa timu hiyo.

 

“Kulikuwa na mambo ambayo yalinifanya kuchukua maamuzi ya kuondoka, kama huna furaha namna nzuri ya kufanya ni kuondoka, sikuondoka kwa ubaya ndiyo maana niliwatakia kila la kheri,” alisema.


“Nachoweza kusema ni kwamba mashabiki wanisamehe kwa sababu kilichotokea ni sehemu ya maisha kwangu mpira ni kazi, unafanya niendeshe maisha yangu,” alisema Mazingisa.

 

Mtendaji huyo wa zamani wa Simba, amerejea nchini jana akitokea kwao Afrika Kusini kwa mapumziko.

 

“Nimekuja Tanzania kuchukua majukumu yangu mapya kwenye klabu yangu ya Yanga,” alisema.

 

Akijibu kuhusu tuhuma ambazo zimetolewa Agosti 20, 2020 na Mwenyekiti wa Bodi wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, alipohojiwa kwenye kituo cha habari cha Wasafi kuwa hakutimiza majukumu yake ikiwemo kubana matumizi na kuamua kujiuzulu, amesema uongozi unajua ukweli akiwemo Mo Dewji.

 

Senzo amesema alipojiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu mara tatu mfululizo alipanga bajeti na Mo Dewji na bodi nzima na kitendo cha kusema mbele ya umma hajatimiza malengo siyo suala la kiungwana.

 

“Sikutegemea iwe hivyo, sipendi kuwe na ubaya baina yangu na waajiri wangu wa zamani, ni vibaya kuwa hivyo, ripoti yangu ya mwisho kuiwasilisha inaonyesha nimetimiza malengo yangu, nimefanya kile kilichopo kwenye bajeti na hela imepatikana. Ripoti itamuonyesha ukweli wote,” alisema.

 

Ameongeza kuwa siyo rahisi kwenda kwenye klabu na kuanza kuzalisha hela haraka bali inatakiwa kujenga msingi, kuhakikisha misingi inakuwa vizuri na mifumo yote imekaa sawa kisha msimu unaofuata ndiyo uanze kuingiza hela,  ila bahati mbaya hakuendelea.

 

Senzo amesema Luis ana mkataba wa miaka mitatu na nusu kuitumikia klabu hiyo.

 

“Ilikuwa shughuli kumpata Luis ila sitazungumzia kuhusu klabu yangu ya zamani ila nitajizungumzia mimi kama niliyehusika kumleta; nasema ni mchezaji wa Simba kwa miaka mitatu na nusu,” alifafanua.

Leave A Reply