The House of Favourite Newspapers

Serikali Kuipatia Bugando Bilioni 4 ya Vifaatiba – Video

0

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kanda ya Bugando, Dk Fabian Massaga amesema hospitali hiyo inatarajia kupokea Sh4.2 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa chumba cha wagonjwa mahututi.

 

Pia fedha hizo zitatumika kununua vifaa kwa ajili ya chumba cha dharula na wagonjwa mahututi, mashine ya X-ray ya kidigitali na mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni.

 

Dk Massaga amesema hayo leo Novemba 18, 2021 katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa hospitali ya Bugando mwaka 1971. Kwamba, fedha hizo ni miongoni mwa zile zilizotolewa kutoka katika mkopo wa IMF ambazo Rais Samia Suluhu Hassan alizipata.

 

“Hili litaboresha huduma zetu. Hospitali hii inahudumia zaidi ya wananchi milioni 18. Aidha inahudumia watu 1400 kwa siku idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na miaka ambayo hospitali hii imefanya kazi,” alisema Dk Massaga.

 

Amesema ikiwa inaadhimisha miaka 50, hospitali hiyo inajivunia hatua kubwa katika utoaji wa huduma za tiba na upasuaji katika kiwango cha ubingwa na ubingwa bobezi.

 

“Hospitali imeendelea kuendesha mafunzo na tafiti mbalimbali ili kuboresha matibabu kwa wakazi wa kanda ya ziwa na tafiti mbalimbali zinazofanyika; miongoni mwake ni kubaini vyanzo vya magonjwa kama saratani, kisukari na shinikizo la damu.

 

“Kupitia tafiti hizi tukishirikiana na chuo kikuu cha CUHAS tulifanikiwa kumgundua mdudu mpya aitwaye Bugandesis ambaye husababisha maambukizi ya damu kwa watoto wachanga. Ni matumaini yetu miaka 50 ijayo hospitali yetu itakuwa na hadhi ya kimataifa yenye uwezo mkubwa wa kuhudumia watanzania kutoka nchi jirani katika ngazi ya utalii wa kimatibabu,” amesema Dk Massaga.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, amesema kanisa na Serikali kushirikiana kutoa huduma ya afya katika eneo hilo imeonyeha mapendo kamili kwa wananchi wanaopata huduma katika eneo hilo.

Leave A Reply