Watuhumiwa Watatu wa Ugaidi Waliotoroka Gerezani Wakamatwa

Msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa watatu wa ugaidi waliotoroka katika Gereza la Kamiti nchini Kenya, umezaa matunda baada ya watuhumiwa hao kukamatwa katika kijiji kimoja ndanindani mwa kaunti ya Kitui, leo Novemba 18, 2021.

 

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kitui, Leah Kithei amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kueleza kwamba walikuwa kwenye hali ya tahadhari kubwa baada ya baadhi ya raia kutoa taarifa ya kuwaona watuhumiwa hao.

 

Awali, taarifa kutoka kwa wananchi wa Kitui, zilieleza kuwa watuhumiwa hao wameonekana katika eneo la maduka la Malalani, Kilometa 100 Mashariki mwa Mji wa Kitui karibu na Mto Tana Kitui na kwamba walinunua kiwango kikubwa cha maziwa, maji, mikate na biskuti ambapo walifanya malipo yote kwa fedha taslimu.

 

Watuhumiwa hao, Musharaf Abdalla Akhulunga maarufu Zarkawi au Alexi, Mohamed Ali Abikar na Joseph Juma Odhiambo maarufu Yusuf walitoroka kutoka katika gereza lenye ulinzi mkali la Kamiti jumapili iliyopita na kuzua taharuki kubwa.

 

Zawadi nono ya Tsh bilioni 1.23 ilitangazwa kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwao huku mkuu wa magereza nchini humo, Wycliffe Ogalo akifutwa kazi na Rais Uhuru Kenyatta na kukamatwa muda mfupi baadaye, kwa tuhuma za kuhusika na njama za kuwatorosha watuhumiwa hao.


Toa comment