The House of Favourite Newspapers

Shamsa Ford: Maneno haya ni akili zako au za kuazima?

0

shamsa-1Staa wa filamu Bongo, Shamsa Ford.

NIANZE kwa kukiri kwamba ninamzimia sana Shamsa Ford awapo kazini. Kwangu ni mmoja kati ya wadada wachache wanaojitahidi kufanya vizuri katika tasnia ya filamu kwa hapa kwetu Bongo.

At least, anaweza kuigiza kile kilichokusudiwa, anashangaa panapostahili mshangao, siyo kama wale wengine wanaotushangaza kwa jinsi wanavyoshangaa. Nimemuona katika filamu kadhaa na kujiridhisha kuwa angalau anaingia katika orodha ya wasichana wachache wanaoweza kufika mbali endapo wataongeza bidii.

shamsa

 

Kama mastaa wengine wa Kibongo, Shamsa naye yumo katika matukio, leo utamsikia kafanya hivi, kesho kaibuka kule ilimradi dunia inaelewa kuwa msichana huyu yupo na anapatikana!

Na katika tokeatokea yake hiyo, juzikati alionekana katika runinga moja ya nyumbani akifanyiwa mahojiano. Alizungumza mambo mengi kuhusu kazi zake. Nilivutiwa na kitu kimoja ambacho niliona ni vizuri kama nitapata nafasi ya kuzungumza naye kupitia safu hii, kwani hii hasa ndiyo sehemu ninayoweza kushiriki naye.

Kati ya mengi aliyoongea, mojawapo lilikuwa ni jinsi maisha yake ya ndoa yalivyokuwa. Itakumbukwa, Shamsa aliwahi kuolewa na mtu mmoja anayejulikana kama Dicky, ambaye baadaye waliachana kwa sababu wanazozijua wao.

Katika kile ambacho watoto wa mjini wanasema, Shamsa ‘alimchana’ vibaya mumewe huyo wa zamani, akimuelezea kwa namna isivyofaa, jinsi maisha yao ya kinyumba yalivyokuwa. Alitoa siri nyeti, ambazo katika hali ya kawaida, mtu aliyestaarabika asingeweza kuzianika katika runinga.
Yaani ilifika wakati nikajiuliza; ni akili zake au aliziazima tu siku ile?
Najua kama Shamsa ni mtoto wa mjini na alidhamiria kufanya kama alivyofanya ili kumtoa ‘nishai’ jamaa.
Sina uhakika ni kwa namna gani binti huyu alivyo na hasira na mumewe wa zamani, lakini cha uhakika kabisa ni kwamba kumbe Shamsa ni ukubwa wa mwili tu, akili zake bado hazijapata utu uzima tunaoutegemea kuwa nao.

Mtu mzima hawezi kuamka asubuhi na kwenda hadharani kuanika mambo yake ya ndani, iwe katika uhusiano wa sasa au wa zamani. Mbaya zaidi, ni pale unapomponda mtu wako, ambaye wakati fulani katika maisha yako, uliwahi kumuona kama sehemu ya mwili wako.

Huu ni ulimbukeni ambao mtu kama Shamsa hafai kuwa nao. Licha ya kwamba muigizaji huyo ni mama, lakini kwa kazi yake, yeye pia ni mwalimu. Anamfundisha mwanaye na mashabiki wanafunzi wote wanaomtazama kwamba mara tu unapoachana na mwenza wako katika uhusiano ni jambo la kawaida kumwaga siri zote za ndani zinazomhusu.

Itakuwaje jamaa naye ‘akifuatwa’ na chombo kingine cha habari halafu akaanika upungufu wa Shamsa ndani ya ndoa?

Kuna tatizo kubwa kwa mastaa wetu wa Bongo, ambao bahati mbaya wamekosa somo la namna gani ya kuishi na umaarufu. Mtu akishapata jina ni kama anapoteza uwezo wake wa kupambanua mambo.
Labda katika kumsaidia tu uelewa ni kwamba maisha ya ndoa yana misukosuko mingi isiyoisha. Ni ndoa chache mno zinazoweza kujigamba kuwa zenyewe ni bora, hazina kasoro.

Kuna udhaifu mkubwa baina ya wanandoa katika jamii yetu, lakini utamaduni wetu hauturuhusu kuropoka mambo ya ndani hadharani. Hii inabaki kuwa siri ya wanandoa na kama kuna mtu mwingine anatakiwa kujua, basi atakuwa mtu ambaye pande zote mbili zinamwamini, awe mzazi, mlezi au msuluhishi.

Na kutokana na hilo, jamii yetu humdharau mtu anayeropoka mambo yake ya ndani, badala ya kumsifia kama ambavyo Shamsa atakuwa anajidanganya. Wanamdharau kwa sababu hata wao wana matatizo katika ndoa zao, lakini wamekaa kimya!

Leave A Reply