Sheria Ngowi Aiomba Serikali Ipunguze Uingizwaji wa Mavazi ya Nje
MBUNIFU maarufu wa mavazi na mitindo wa kitaifa na kimataifa, Sheria Ngowi, ameiomba serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo kupunguza uingizwaji wa mavazi ya nje.
Sheria amesema jambo hilo litasaidia kuinua soko la wabunifu wa mavazi wa ndani ya nchi ili kukuza kipato na pato la taifa kwa ujumla.
Sheria amesema jambo hilo litasaidia kuinua soko la wabunifu wa mavazi wa ndani ya nchi ili kukuza kipato na pato la taifa kwa ujumla.
Mkali huyo wa mavazi amesema kuwa bila serikali kuweka mkono wake katika masuala ya sanaa, wasanii hawatafikia malengo kutokana na masoko yao kuyumba.
Aidha, amesema ni vizuri likawepo Vazi Rasmi la Taifa ili kuweza kuwatambulisha Watanzania pale linapokuja suala la ubunifu kwani kila kabila hapa nchini lina vazi lake rasmi la asili, hivyo ingependeza kuwepo na vazi la taifa litakalowakilisha mavazi ya makabila yote.
Pia, mbunifu huyo amewashauri vijana kuendelea kujituma katika kutimiza ndoto zao na kutoogopa changamoto ambazo wanakutana nazo katika kutimiza ndoto zao.
Amesema yeye binafsi ni mmoja kati ya watu ambao kwa miaka saba ameweza kufanya kazi za ubunifu na ameshikilia nafasi ya kwanza Barani Afrika na kuchukua tuzo za ubunifu wa mavazi duniani mara 44.
PICHA NA HUSSEIN MANANE | +255 GLOBAL RADIO