The House of Favourite Newspapers

Yanga Yamshusha Kocha Mpya Msauzi

0

WANACHOKIFANYA Yanga ni kutengeneza bomu! Ndivyo unavyoweza kusema kwani baada ya Alhamisi iliyopita kumleta Kocha Mkuu Luc Eymael raia Ubelgiji, jana Jumapili wakamalizana na kocha mwingine, Riedoh Berdien ambaye anakuja kwa kazi maalumu ya kuwaweka fiti mastaa wa timu hiyo.

 

Yanga wamemleta kocha huyo raia wa Afrika Kusini ambaye muda wowote kutoka leo Jumatatu atatua nchini kwa ajili ya kuanza kazi baada ya dili lake kukamilishwa nchini Afrika Kusini.

 

Dili hilo limekamilishwa na wadhamini wa Yanga, Kampuni ya GSM chini ya Mkurugenzi wa Uwekezaji, Injinia Hersi Said ambaye amehusika katika kufanikisha madili yote kuanzia makocha hadi wachezaji.

 

Berdien anakuja kwa kazi mbili maalum ndani ya Yanga, ambapo kazi ya kwanza ni kuwa kocha wa fitinesi lakini kazi ya pili kuwa kocha wa pili msaidizi ambaye atasaidiana na mzawa Charles Mkwasa kumshauri bosi wao Eymael.

 

Inavyoonyesha dili la kuletwa kwa Berdien limesimamiwa na Eymael kutokana na wawili hao kufanya kazi kwa pamoja walipokuwa Afrika Kusini.

 

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amelithibitishia Gazeti la Championi Jumatatu, kuwa wamefikia makubaliano mazuri na kocha huyo na muda wowote atatua nchini kwa ajili ya kuungana nao kuanza majukumu yake.

 

“Tumefikia makubaliano mazuri na kocha huyo na muda wowote kuanzia kesho (leo) atatua nchini kwa ajili ya kuanza majukumu yake. Kila kitu kilimalizwa kule Afrika Kusini na kinachosubiriwa ni kocha tu kuja kuanza kazi,” alisema Mwakalebela.

 

Rekodi za Berdien mwenye beji ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) zinaonyesha kuwa ameshafanya kazi katika klabu za Free State Stars na Chippa United ya Afrika Kusini, timu za taifa za Botswana, Bangladesh, Trinidad and Tobago na timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini (Banyana Banyana).

SAID ALLY NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply