The House of Favourite Newspapers

Shigongo: Nitaleta Greda Zangu Kutengeneza Barabara Buchosa – Video

0
Mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo,  akionyesha ilani ya chama hicho yenye sera atakazozitekeleza iwapo wananchi watampa ridhaa.

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Buchosa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James, ameendelea kuchanja mbuga kwenye kampeni za kunadi sera zake na chama chake akiomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo ili waweze kumpa ridhaa ya kuwa mbunge wao kwa miaka mitano ijayo.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kazunzu jana jioni Oktoba 2, 2020, ambapo amefanya mikutano yake katika vijiji vitatu vya, Ilyamchele, Kasaraji na Nyambeba, Shigongo amesema kuwa kabla ya kuchukua uamuzi huo alijitafakari, akajipima na kuona anafaa kuwatumikia wananchi hao kutokana na mapenzi mema aliyo nayo kwao na kwa taifa na kuongeza kuwa uwezo anao wa kuhakikisha anafanya kila atakaloweza ili kuwaletea maendeleo wananchi hao.

…Akimwombea kwa wananchi mgombea udiwani wa Kata ya Kazunzu kupitia CCM, Boniphace Msenyelwa Maseswa.

Shigongo amewaahidi wananchi hao kuwa iwapo atachaguliwa kuwa mbunge atahakikisha anawaletea maendeleo ambayo hawajawahi kuyapata kutokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliwa nazo hususani katika elimu, afya na  kuwainua kiuchumi.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nyambeba kata ya Kazunzu wakifuatilia mkutano wake.

“Nitafanya kazi kubwa na nyinyi kwa miaka mitano, nimewaaga wafanyakazi wangu nije huku Buchosa niwatumikie, nionyeshe maana ya uongozi kwamba ni kuwatumikia wananchi na si vinginevyo, nitahakikisha tunafanya kazi kwa pamoja ili tujiletee maendeleo,” alisema Shigongo.

Amewataka siku ya  Oktoba 28 mwaka huu wampatie kura za ndiyo Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mbunge na madiwani wote wa CCM.

…Akiwahutubia wananchi wa   Nyambeba.

Shigongo amesema iwapo atachaguliwa atawatumikia wana-Buchosa kwa unyeyekevu mkubwa kwa kushirikiana na wananchi hao katika kuleta maendeleo ya mtu mmoja-mmoja na jamii nzima ya wana-Buchosa.

Baadhi ya wanakikundi cha kwaya wakiimba nyimbo  za kuhamasisha kampeni.

 

Katika kutimiza ndoto hiyo, Shigongo amesema ili kufikia malengo  atazunguka jimbo zima kufundisha namna ya kutoka kwenye hali duni ya maisha ili kujikwamua sambamba na kuboresha elimu katika shule za msingi na sekondari kwa kushirikiana na wanachi kujenga madarasa, vyoo, nyumba za walimu na kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu ili watoto waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.
#chaguaShigongo

Kwa upande wa miundombinu,  amesema ili kuboresha barabara za vijiji endapo wakimchagua atanunua magreda yake binafsi ili kazi ya kutengeneza barabara iwe rahisi.  Pia ameahidi kuendeleza vipaji vya sanaa na michezo katika jimbo hilo kwa kuanzisha mashindano mbalimbali ya kuibua vipaji ikiwemo kurudisha mashindano ya Shigongo Cup na matamasha mengi ya kuibua vipaji vya muziki na fani mbalimbali.

 


Leave A Reply