The House of Favourite Newspapers

Shigongo Awataka Wafungwa Ukonga Kutokata Tamaa

14692131_1154273521331558_3945318408192779795_o

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, Eric Shigongo.

Na Sweetbert Lukonge

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, Eric Shigongo, amewataka wafungwa wanaotumikia vifungo vyao katika Gereza Kuu la Ukonga jijini Dar es Salaam kutokata tamaa ya maisha.

Shigongo aliyasema hayo wakati alipoungana na wafungwa hao leo Ijumaa katika tamasha lililoandaliwa na Kampuni ya Global Publishers la kuadhimisha miaka 17 ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika kwenye viwanja vya ndani ya gereza hilo.

Aliwataka wafungwa hao kujua kuwa katika maisha hakuna mtu yeyote aliyeumbwa na Mungu anayejua hatima ya maisha yake ya baadaye, hivyo wanapaswa kutokata tamaa.

“Kama alivyofanya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kila mmoja wenu ana uwezo wa kufanya kama yeye, mna uwezo wa kubadilisha maisha yenu kwani hukumu ya mwanadamu isiwe sababu ya kuwakatisha tamaa kabla ya hukumu ya mwenyezi Mungu.

“Natambua kuwa mmeitwa majina mengi lakini hiyo isiwe sababu ya kuwakatisha tamaa ya maisha, hapa duniani wapo watu wengi ambao walikuwa kama ninyi lakini baada ya kumaliza vifungo vyao na kurudi uraiani hivi sasa ni mamilionea kwa sababu tu hawakukata tamaa,” alisema Shigongo ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo.

 

Comments are closed.