The House of Favourite Newspapers

SHILOLE; KUTOKA MUUZA GENGE HADI BOSS LADY

Zuwena Mohamed ‘Shilole’

BOSS LADY ni jina ambalo si vibaya ukimuita mrembo Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ambaye historia ya maisha yake ina fundisho kubwa kutokana na jinsi alivyopambana hadi kufikia mafanikio aliyonayo.  Mrembo huyu ambaye historia yake ya umaarufu ilianzia kwenye uigizaji, amepambana na kufanya vizuri pia kwenye ulimwengu wa muziki wa Bongo Fleva ambao umezaa pia miradi mbalimbali ikiwemo mgahawa.

Kwenye mgahawa wake huo uliopo maeneo ya Morocco jijini Dar, Shilole ameajiri wafanyakazi wasiopungua kumi wakifanya biashara ya chakula na kutengeneza fedha.

ALIANZIA WAPI?

Shilole alizaliwa Igunga, Mkoa wa Tabora mwaka 1987 ambapo alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Igunga na alipata nafasi ya kuendelea na masomo lakini kwa bahati mbaya aliishia kidato cha baada ya kubakwa alipokuwa anaenda kisimani kuchota maji. Shilole alifikia hatua hiyo baada ya kupewa ujauzito wa mtoto wake wa kwanza anayeitwa Joyce, hapo ndipo ndoto za mpambanaji huyo zili pozimika jumla.

AANZA MAPAMBANO

Baada ya kujifungua, Shilole aliingia barabarani kwenye stendi ya mabasi ya mikoani Igunga, akiwa na umri wa miaka 15. Kwenye stendi hiyo aliuza mikate na maji ya kunywa kwa abiria ambao wanatoka mikoani huku mikate mingine akitembeza majumbani kwa watu ili aweze kujipatia riziki yake, mwanaye na familia pia.

Baada ya kipato kidogo kuongezeka, alifungua genge lake na kufanikiwa kuhamia kwenye chumba chake kwa kumudu kulipia kodi kwa kulipia kodi ya shilingi 3000 kwa mwezi, alikaa hapo kwa takriban miaka miwili.

SAFARI YA DAR

Akiwa anahangaika na maisha, Shilole alipata mwanaume mwingine akiwa na umri wa miaka 17, ambaye alitokea kumpenda, akamtolea posa nyumbani kwao, akamuoa kisha kumchukua na kuja naye jijini Dar, hiyo ilikuwa ni mwaka 2005. Kwa mara ya kwanza walifikia gesti lakini baadaye mwanaume huyo alitafuta nyumba na kuanza kuishi naye pamoja.

WAMWAGANA

Badaa ya kuishi na mumewe huyo kwa muda, alimpa ujauzito wa mtoto wake wa pili ambapo alijifungua salama lakini baada ya muda, mumewe huyo alianza kubadilika tabia kwani alianza kumpiga sana Shilole. Mara kadhaa mrembo huyo alilazimika kulala na watoto katika Kituo cha Polisi Keko hadi pale alipojiongeza kwa kutafuta chuo cha Hotel Management japo mumewe huyo hakupenda na alipohitimu alipata kazi Peak Cock Hotel na mumewe alivyoona hivyo alimpa talaka.

AKUTANA NA RAY

Akiwa anaendelea kufanya kazi hotelini hapo muigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’ alifika kupata huduma na ndipo alipovutiwa na uchangamfu wake hivyo walivyozoeana, Shilole akamwambia anapenda kuigiza ndipo alipompa nafasi ya kuigiza filamu ya kwanza inayoitwa Fair Decision na hapo ndipo ukawa mlango wa mwanamuziki huyo kutoka kwenye upande wa filamu.

AFUNGUA DUKA LA NGUO, PUB

Wakati akiwa kwenye filamu, aliamua kufungua duka dogo la nguo maeneo ya Mwananyamala- Komakoma ambapo pembeni yake alifungua Pub yake ambayo ilikuwa ikifanya vizuri sana ambapo pesa hizo zilikuwa zikimsaidia kuwasomesha watoto wake na kufanya mahitaji yake.

AKUTANA NA Q. CHIEF

Shilole akiwa katika matembezi, alikutana na mwanamuziki Q. Chief ambapo alimwambia jinsi alivyokuwa na ndoto za kuimba, mwanamuziki huyo akamchukua na kumpeleka Coco Beach kwa ajili ya kumpima kuimba na kumuona kuwa ana kipaji hivyo alimpeleka Studio za C9 Records ambapo alitoa wimbo wake wa kwanza unaoitwa Lawama na baadaye alienda kuonana na Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba ambaye alimpa moyo na kuanza kutoa nyimbo nyingine kisha akaanza kupata shoo mbalimbali.

AFUNGUA MGAHAWA

Baada ya maisha yake kunyooka zaidi, Shilole aliamua kujiongeza kwa kufungua mgahawa mkubwa ambao unaitwa Shishi Food na mpaka sasa unafanya vizuri huku akishirikiana vizuri na mume wake mpenzi Uchebe.

NI BOSSLADY

Mpaka sasa mbali na kupiga shoo mbalimbali, mgahawa huo unampatia fedha nyingi Shilole na anaendesha maisha yake vizuri kwani tayari ameshajenga nyumba kubwa, anamiliki gari aina ya Toyota Rush huku watoto akiwasomesha shule nzuri.

Comments are closed.