The House of Favourite Newspapers

Shilole + Uchebe = Mapacha wa Mwendokasi

0

ZUWENA Yusuph Mohammed almaarufu kama Shilole au Shishi Baby au Shishi Trump, ‘haso’ zake zinajulikana. Si za kitoto!

 

Kutoka kijijini Igunga mkoani Tabora alikoishi maisha mabaya kutokana na umaskini na kutelekezwa na mwanaume, kisha kuwa mhudumu migahawani na mahotelini kabla ya kuzama kwenye tasnia ya filamu za Kibongo, Bongo Fleva na ujasiriamali, hii ni sehemu ndogo tu ya utambulisho wake, mengine aliyopitia tunaweza kujaza ukurasa huu.

 

OVER ZE WEEKEND wiki hii imetua kwenye ‘kapo’ ya mwanamama huyu na mumewe, Ashraf Uchebe.

Ni miaka minne sasa tangu wawili hao walipofunga ndoa, lakini mapenzi yao yanatajwa kunawiri siku hadi siku.

 

OVER ZE WEEKEND imepiga stori na Shilole na Uchebe ambapo wanafunguka kwamba, ndiyo kwanza gari limewaka na unaweza kusema penzi lao ni la mwendokasi.

OVER ZE WEEKEND: Nini siri ya kudumu kwenu, kwani tunaona ndoa nyingi za mastaa zikivunjika zikiwa changa kabisa?

 

SHILOLE: Kwanza nimeshakuwa mtu mzima (amezaliwa Desemba 20, 1987). Nina watoto wakubwa sasa (ana watoto wawili aliozaa na wanaume tofauti; siyo Uchebe).

Nimepitia changamoto nyingi za kimaisha, hivyo kama unakutana na mtu anakupa sapoti kubwa kwenye maisha yako, kwa nini ujitoe ufahamu? Siri kubwa ya maisha yetu ni kuelewana na kujuana kila kitu. Mmoja akizingua, tunapeana ukweli kisha maisha yanaendelea.

 

OVER ZE WEEKEND: Kuna madai kwamba, una mkono mwepesi wa kupiga mtu, vipi hakuna ngumi?

SHILOLE: Baadhi ya watu wanapoona mapenzi ya watu yanakwenda vizuri, hawaachi kutia maneno yao mengi, mara utasikia fulani anapigwa, lakini kama Uchebe ananipiga, ni mahaba tu na si kitu kingine.

 

OVER ZE WEEKEND: Inasemekana una wivu sana kwa Uchebe, hili limekaaje?

SHILOLE: Ukisikia wivu, basi ujue hapa ndipo penyewe. Unajua kwa nini? Ni kwa sababu ninampenda sana na yeye anajua hivyo.

OVER ZE WEEKEND: Uchebe anakusapoti kiasi gani kwenye biashara yako ya huduma ya chakula?

 

SHILOLE: Kiukweli yupo mstari wa mbele sana katika kunisapoti kwenye biashara zangu. Nakumbuka zamani alikuwa akishinda na mimi hata kwenye biashara yangu, tunapika wote na tunakaa wote hadi jioni.

 

OVER ZE WEEKEND: Unazungumziaje ubabe kwa mumeo? SHILOLE: Thubutuuu…ninaanzaje kuwa mbabe kwa mume wangu? Kwani tatizo ni nini mpaka niwe hivyo? Nitafanya yote, lakini siyo ubabe kwa mume wangu. Nioneni hivihivi, lakini mbele ya mume wangu nina heshima debe.

 

OVER ZE WEEKEND: Baadhi ya jamii zetu ndoa ikichelewa kujibu kunakuwa na maneno mengi hasa upande wa kiumeni, je, ndoa yenu itajibu lini?

SHILOLE: Siwezi kusema ninatarajia lini, nasubiri tu Mungu aweke mkono wake, lakini wakati wowote akijibu maombi yetu, nitamzalia mume wangu japokuwa tuna watoto.

 

OVER ZE WEEKEND: Kwa upande wako Uchebe, unamzungumziaje Shilole?

UCHEBE: Ni zaidi ya mke kwangu, ananiheshimu sana, anajua maisha, anajua kutafuta na ni mwanamke mwenye akili mno. Sijui nisemeje, lakini kwa upande wangu nina almasi ndani.

 

OVER ZE WEEKEND: Umewezaje kumkataza Shilole mambo ya ulevi na nguo fupi?

UCHEBE: Jambo lolote halihitaji haraka, nilijua tu ipo siku mke wangu atabadilika, leo anaswali na wala hagusi kitu kinachoitwa pombe.

 

OVER ZE WEEKEND: Vipi kuhusu kumpa kichapo?

UCHEBE: Hata kofi sijawahi kumpiga. Kwa nini nifanye hivyo? Mke wangu ni msikivu na mwelewa sana kama unamwelekeza kitu.

OVER ZE WEEKEND: Ni kweli kwa Shilole ndiyo umefika?

 

UCHEBE: Kama uliwahi kusikia meli imetia nanga, basi na mimi ndiyo nimetia nanga. Sina mpango wa kubanduka kwenda popote, yaani sisi ni mapacha na kama ni mapenzi, ya kwetu ni ya mwendokasi.

 

OVER ZE WEEKEND: Kuna maneno kwamba, wewe ni mdogo kiumri kwa Shilole, je, ni kweli?

UCHEBE: Wanaangalia nini? Mwili wangu? Hata kama ningekuwa mdogo, nikishaitwa mume, basi mimi ni mkubwa. Watu wasiangalie mwili wangu mdogo, Shilole kwangu ni kama mtoto.

Leave A Reply