The House of Favourite Newspapers

Shinikizo la Damu (Hypertension)-2

0

Shinikizo la damu limegawanyika katika makundi mawili, aina ya kwanza ambalo kitaalam huitwa Primary au Essential Hypertension. Aina hii ya shinikizo la damu huwapata asilimia 90 hadi 95 ya wagonjwa, huku sababu zikiwa hazijulikani suala linalomaanisha kuwa wagonjwa huwa hawana sababu za wazi zinazosababisha tatizo hilo.

Kesi zinazobakia za shinikizo la damu ambazo ni asilimia 5-10 za wagonjwa husababishwa na shinikizo la damu aina ya pili, na kitaalam huitwa Secondary Hypertension.

Aina hii husababishwa na sababu mbalimbali zinazotokana na matatizo ya figo, mishipa ya damu, moyo na mfumo wa Endocrine. Shinikizo la damu kwa kawaida huongezeka katika kipindi cha miaka kadhaa na huweza kumpata karibu kila mtu, lakini huwapata zaidi watu wazima wenye umri wa zaidi ya miaka 35.

Mambo mengi huchangia ugonjwa wa shinikizo la damu kama vile kiwango cha maji na chumvi mwilini, homoni, mishughuliko ya mtu, hali ya joto au hali ya baridi, hisia, hali ya figo, mfumo wa neva na mishipa ya damu.

Iwapo shinikizo la damu litakuwa juu na kuachwa bila kudhibitiwa, moyo na mishipa ya damu hushindwa kufanya kazi ipasavyo. Kwa bahati nzuri, shinikizo la juu la damu ni rahisi sana kugunduliwa, kutibiwa na kudhibitiwa.

HUSABABISHWA NA NINI?

Pengine wengi tunajiuliza kuwa shinikizo la damu husababishwa na nini. Jibu ni kuwa, kuna sababu nyingi zinazotofautiana kulingana na aina ya ugonjwa huo. Katika aina ya kwanza ya shinikizo la damu ingawa chanzo huwa hakijulikani, lakini sababu za kijenetiki na za kimazingira kama chakula na mazoeni zina nafasi muhimu katika usababishaji wa ugonjwa huo.

Hivyo masuala yafuatayo yamehusishwa katika kusababisha aina hii ya shinikizo la damu.

Masuala hayo ni uvutaji sigara, unene (visceral obesity) yaani unene wa sehemu za tumbo, unywaji pombe, upungufu wa madini ya potassium, upungufu wa vitamin D, kurithi, umri mkubwa, chumvi na madini ya sodium kwa ujumla, ongezeko la kemikali kwenye figo (renin) na kushindwa kufanya kazi kichocheo cha insulin.

Aina ya pili ya shinikizo la damu husababishwa na tatizo lililopo mwilini. Matatizo hayo ni pamoja na kasoro ya kuzaliwa nayo katika mshipa mkubwa wa damu, saratani ya figo, saratani ya tezi iliyo juu ya figo, hali ya kushindwa kupumua vyema usingizini (sleep Apnea), ujauzito ambapo baadhi wajawazito hupata shinikizo la damu suala linalosababisha hatari ya  kupata kifafa cha mimba (eclampsia).

Pia magonjwa ya figo kama vile mshipa wa damu wa figo kuwa mwembamba yaani renal artery stenosis, matumizi ya baadhi ya dawa, madawa ya kulevya au kemikali,  na kadhalika.

DALILI ZAKE

Mgonjwa anaweza huhisi hali zifuatavyo. Uchovu, maumivu ya kichwa, mapigo ya moyo kwenda mbio, kichefuchefu, kutapika, damu kutoka puani, kutoona vizuri (blurred vision), kupauka kwa ngozi au kuongezeka wekundu wa ngozi, kuhisi hali ya woga, kusikia kelele masikioni na mara chache kuchanganyikiwa.

Pale mtu anapokuwa na dalili za shinikizo la damu hupaswa kufanyiwa uchunguzi na vipimo vifuatavyo ili kuhakikisha kwamba ana tatizo hilo.

Ni muhimu kupimwa shinikizo la damu mara kwa mara (angalau mara moja kila baada ya mwaka mmoja au miwili). Unashauriwa kutokunywa vinywaji vyenye kafeini au kuvuta sigara kabla ya kupimwa shinikizo la damu.

Kama shinikizo lako la damu liko juu, ni muhimu kumuona daktari ili kuweza kufanyiwa uchunguzi zaidi wa matatizo ya kiafya. Kipimo kimoja cha shinikizo la damu hakimaanishi kupatikana au kuugua ugonjwa huo, na inabidi kupimwa zaidi ya mara mbili.

Huhitajia kupimwa angalau mara tatu tofauti, kwa wiki moja ili kuthibitisha kwamba mtu ana ugonjwa huo kwa kutumia kifaa maalumu cha kupimia shinikizo la damu kinachoitwa Sphygmomanometer.

Vipimo vingine ni pamoja na kuchunguza damu ili kufahamu wingi wa cholesterol mwilini na pia kupimwa BUN na electrolytes. Kipimo kingine ni cha kuchunguza mkojo, ECG, Echocardiography na pia Ultrasound ya mafigo.

MATIBABU YAKE

Baada ya vipimo kunyesha kuwa mgonjwa ana shinikizo la damu matibabu hufuata. Lengo la matibabu ni kuzuia madhara ambayo yanaweza kuletwa na shinikizo la damu.

Kuna dawa mbalimbali zinazotumika kutibu shinikizo la damu kama dawa jamii ya Alpha blockers, dawa jamii ya Angiotensin converting enzyme inhibitor (ACEI), dawa jamii ya Angiotensin receptor blocker (ARB), dawa jamii ya Beta blocker, dawa jamii ya Calcium channel blocker, dawa jamii ya Diuretics yaani zile zinazopunguza maji mwilini au kuongeza mkojo, dawa jamii ya Renin inhibitors na pia Vasodilators.

Wapenzi wasomaji inafaa kujua kuwa, shinikizo la damu lisipotibiwa na kudhibitiwa husababisha madhara mbalimbali.

Madhara hayo ni kama vile kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi, matatizo katika mshipa mkubwa wa damu ambapo ukuta wa ndani huchanika na damu kukusanyika katika ukuta wa mshipa huo, magonjwa ya mishipa ya damu, kushindwa kuona na pia huathiri ubongo.

USHAURI

Mbali na kutumia dawa tulizozitaja, tunashauri kuwa  tunaweza kuzuia na kudhibiti shinikizo la damu kwa njia tofauti ambazo ni:

1) Kula lishe bora na chakula kusichokuwa na mafuta mengi, na pia chenye madini ya potassium kitaalamu kinaitwa DASH diet ambacho ni maalumu kwa ajili ya kuzuia shinikizo la damu.

2) Kufanya mazoezi mara kwa mara, angalau nusu saa kwa siku.

3) Kuacha kuvuta sigara na kunywa pombe kwa wale wenye tabia hizo.

4) Kupunguza utumiaji wa chumvi nyingi katika chakula hasa ya kuongezea mezani (tunapaswa kutotumia zaidi ya gramu 1.5 ya chumvi kwa siku).

5)  Kupunguza msongo wa mawazo na kuhakikisha kuwa tunakuwa na uzito unaotakiwa kiafya kulingana na kimo, na kama tuna uzito uliozidi tunapaswa kupunguza uzito huo ili uwe katika kiwango kinachotakiwa

6) Kula samaki au kutumia mafuta ya samaki ambayo husaidia kupunguza shinikizo la damu, kwa wenye shinikizo la damu.

Tukutane wiki ijayo kwenye gazeti hili hili.

Leave A Reply