The House of Favourite Newspapers

SHOGA; Chakula cha Jirani Hakina Ladha

Na MWANDISHI WETU| GAZETI LA UWAZI| MAKALA

MMH! Makubwa haya shoga yangu na madogo yana nafuu! Basi mwakwetu kuna watu hawana haya, waliopinda wakapinduliwa tangu udogoni na kujifi cha katika mavazi ya heshima na maneno matamu, lakini tabia zao ni kutwa kukimbilia na kula chakula cha jirani yaani wamekuwa kama rangi ya kaniki hata ukifua vipi haiwezi kuwa nyeupe kwa vile weusi ni rangi yake ya asili, upo? Looh!

Maana hili la leo limenifi ka hapa!! Nimesahau hata kukusalimu shoga yangu wa ukwee… maana si kwa kuvurugwa huku, yaani kuna watu wanakera ati! U hali gani shoga yangu unayenisoma hapa Jumanne ya leo? Kama ni mzima ni faraja kwangu lakini kama unaumwa nikuombee tu Mwenyezi Mungu akujalie afya njema.

Ujue shoga kuna wanawake wana roho ngumu kama rangi ya kaniki ndiyo maana nilishawahi kumueleza shoga yangu mmoja hivi kuwa asimlaumu dobi kwa rangi ya kaniki kwa kuamini anaweza kuifua na kufanya weusi kuwa weupe. Najua utakuwa unajiuliza shoga leo kaamkaje tena, mbona anazungumza kama siyo kuchonga kwa sana! Tena wengine usikute mmetoa macho pima kutaka kujua na kuniona kama nakulisha chakula cha Kihindi chenye pilipili nyingi au la! Unalo shoga!

Usikonde shoga yangu, mi na wewe tena kama mjusi ndani ya pango la jiwe! Shoga mada ya leo kama nilivyoanza kukuwekea hapo juu kwenye kichwa cha habari. Ujue kuna wanawake wenzetu walio ndani ya ndoa wanafanya vitu vya aibu hadi unabaki unajiuliza kwa nini sasa walikubali kuolewa.

Basi unaambiwa shoga yangu kuna mama mtu mzima aliyetakiwa kutulia ndani ya ndoa yake, amekuwa akimdhalilisha mumewe kwa kukimbilia na kula chakula cha jirani kwa kudhani kina utamu kuliko cha nyumbani kwake.

Shoga yangu mmoja ambaye ni jirani yake na ni mtu wake wa karibu sana, tabia ile ilimchefua sana na kuamua kumwambia anayofanya siyo mazuri kwani anamuaibisha mumewe.

Japo mama huyu mtu mzima anayetakiwa kuwa na wajukuu alisingizia akila chakula cha usiku na mumewe hashibi, loooh, jitu zima ovyoo! Jamani hivi mpaka leo mmezaa na mna watoto, unalishwa chakula siku zote hizo leo hii unasema hushibi? Unataka kuniambia kumpelekea chakula mwanaume wengine huko nje ndo kutakufanya ushibe?

Shoga yangu huyo aliendelea kunipasha kuwa, majibu ya mtu mzima huyo asiye na haya eti amwache yeye kula huko inamhusu nini, kwa vile hicho chakula anatoa yeye wala si cha mtu.

Kama ni hivyo basi vua hiyo hijabu uliyoifanya kichaka cha kukuonesha kondoo, kumbe ndani ni chui mbaya kwa wanaume ili uungane na makahaba wenzako wanaopeleka chakula kwa wanaume wengi kuliko kutudhalilisha wanawake tunaojua nini maana ya chakula cha usiku kwa kuziheshimu ndoa zetu. Najua nimekugusa na wewe mwenye tabia kama hii, ushapinda mdomo kama kiatu cha mwanajeshi mstaafu kilichokwisha, ndiyo tabia yako ya kuwapelekea chakula wanaume wengine kama mapokezi ya nyumba ya wageni kila mgeni lazima ale.

Ni bora basi ukamuweka mzee sawa na kumuambia wapi anakosea ili mrekebishe kuliko kudanganyika kama siyo kukurupuka na kwenda kula huko, hivi hujui chakula hicho kikiingia inzi wengi kitakuletea magonjwa?

Nasema sipendi na sitaki kuisikia tena tabia hii, nasema na wewe unayejijua na kujibu majibu ya kifedhuli tena nakwambia ukome kumdhalilisha mzee. Mbona wenzako wametulia tuli wanakula chakula kwa furaha kwenye ndoa zao kwani hawawezi kuwapelekea majirani wakaonja?

Shoga yawezekana kabisa haya ninayoyasema yataingilia kulia na kutokea kushoto, siwezi kukulaumu kwa vile umeshaharibika ukubwani na tabia yako kama rangi ya kaniki hata ukimaliza bahari nzima na sabuni zote za duniani bado rangi yako itabakia nyeusi. Kwa leo niishie hapa tukutane tena wiki ijayo!

Comments are closed.