Shoga, nyuki mkali kwa asali yake

Shoga naona leo kicheko mpaka gego la mwisho, najua lazima ucheke kwani ndoa yako ilikuwa imesimamia mguu mmoja leo hii imesimamia miguu miwili, hongera.

Inawezekana nawe ulikuwa mmoja wa waliokuwa wakiichukia kona hii na kuona kama inakufuatafuata. Baada ya maji kufika shingoni, mwenyewe umeyatafuta magazeti ya zamani ili kujua umekosea wapi.

Jamani kona hii ipo kwa ajili yetu sote, hata sisi enzi ya ujana wetu tulifanya makosa, lakini walikuwepo wakubwa waliotuweka chini na kutuelekeza tulipoyafuata mambo yalikwenda vizuri. Lakini sasa hivi hakuna mzazi anayepoteza muda kumuweka chini mwanaye  afanye nini. Inawezekana makosa yao ndiyo yanafanya wapate mkate wa kila siku.

Hilo nililiona, ndiyo makusudi ya kuanzisha kona hii yangu mimi Naa, wazazi najua wamewashindwa lakini mimi ni sawa na mtumbua jipu, simuonei huruma mtu. Maneno yangu yanayowachoma moyo ndiyo tiba yenu kama wengine ambao wamesahau maumivu ya ndoa.

Nauliza kuna mtu aliyenitafuta kunipa hata asante ya mdomo? Lakini ndiyo mliokuwa kiherehere kukosoa makala haya.

Jamani leo silo lililonileta, nilitaka kuwakumbusha tu umuhimu wa kona hii, kilicho nichonyota moyoni kinatokana na mkasa wa mtoto wa shoga yangu ambaye aliolewa miaka mitatu iliyopita, nami nilikuwepo kwenye sherehe, nikanywa na kula.

Juzi nilimkuta amejaa tele kama pishi la mchele. Nilijua amerudi kumtembelea mzazi wake, lakini taarifa nilizozipata toka kwa mama yake, eti ameisusa ndoa baada ya kugundua mumewe anatembea na shoga yake.

Kitendo kile kilinishtua sana, mtoto wa kike kuikimbia nyumba yake kwa sababu ya shogae kutembea na mumewe? Sasa nikamuuliza kwa hiyo nyumba kamwachia rasmi shoga yake? Mtoto wa kike akiwa amepandwa na jazba  alisema  eti hawezi kuchangia mume na shoga yake, maneno yake yalinifanya niangue kicheko na kuona kama nimemdharau, lakini lengo langu kumtoa akili kwa maamuzi yake ya kukurupuka.

Jamani tangu lini nyuki akaukimbia mzinga wake kwa sababu mtu katia mkono? Ukiona mtu katia mkono ujue mzinga wako una asali tamu. Sasa wewe unapandwa na hasira za mkizi unampa faida mvuvi. Shoga kwa taarifa yako mapenzi hayasuswi na mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe. Ukiona hivyo usikurupuke kukimbia jiulize umekosea wapi.

Pengine uliyaachia mazoea kati ya shoga yako na mumeo yakavuka mipaka, siku zote nyuki mkali kwa asali yake, hakuruhusu hata kuusogelea mzinga wake. Shoga wengine wapo kwa kazi hiyo, kujirahisi kwa mabwana wa marafiki zao kwa vile wao kwao yamewashinda.  Sawa limekuuma kwa mtu kutia mkono kwenye mzinga wako na kulamba asali yako, unachotakiwa kuangalia umekosea wapi?

Wanawake wengine wana tabia mbaya, pamoja na ushoga wenu unatakiwa umuwekee mipaka, mazoea yakivuka mipaka kati ya mwanaume na mwanamke lazima patafanyika usaliti tu. Pia na sisi wanawake tulioolewa tunajisahau sana, hatujishughulishi kujiweka vizuri kimavazi hata mapambo.

Shogayo kila akija, ananukia utuli, anavaa nguo za mitego, umbile linavutia, mumeo naye anashtuka kwa vile ndani hayo hayaoni. Jamani tujichunguze tabia zetu muonekano wetu wa kujijali kwa mapambo na usafi wa nyumba. Pia kauli zetu zibadilike, mumeo baada ya kazi anataka lugha nzuri ya kumfanya aifurahie nyumba yake.

Tusijisahau kwa vile tumeolewa basi kila kitu kimekwisha, kumbuka wasio na waume ni wengi kuliko walioolewa hivyo inatakiwa muwe nao makini sana kwa kuwalinda  waume zetu. Siku zote mapenzi hayasuswi na nyuki mkali kwa asali yake, usimruhusu mtu auchezee utamu wako.

Yangu kwa leo ni hayo. Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.  


Loading...

Toa comment