The House of Favourite Newspapers

Unending Love

1

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanashangazwa mno na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao.

Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini. Moyo wake unabaki na majeraha makubwa yasiyopona.

Je, nini kitafuatia?

 SONGA NAYO…

Anna, can you be my only Juliet?” (Anna, unaweza kuwa Juliet wangu pekee?) aliuliza William, alikuwa amemshika Anna mkono.

“It’s impossible William,” (Haiwezekani William) alisema Anna kwa sauti ndogo yenye kumaanisha.

“Why?” (Kwa nini?)

“I can’t fall in love, let me be your BFF,” (Siwezi kuangukia kwenye mapenzi, acha niwe BFF wako)

“Best Friend Forever?” (Rafiki wa karibu milele)

“Yes!” (ndiyo)

William akashusha pumzi ndefu. Jibu la Anna, hakika lilimchanganya.

“Ina maana sikuvutii?”

“Sijamaanisha hivyo William, tafadhali usinielewe vibaya.”

“Sasa kwa nini huwezi kuwa mpenzi wangu jamani Anna? Tafadhali naomba nionee huruma. Nateseka mwenzio.”

“Hapana William, naomba unielewe,” alisema Anna lakini tofauti na awali, safari hii uso wake ulikuwa umejawa na huzuni, kwa mbali machozi yakaanza kumlengalenga.

“Ooh! I’m sorry, I didn’t mean to make you sad, I simply wanted to let you know my feelings.” (Ooh! Samahani sana, sikumaanisha kukufanya uwe na huzuni, nilitaka tu kukufanya ujue hisia zangu) alisema William kwa upole baada ya kuona Anna amebadilika kabisa.

Msichana huyo hakujibu kitu, akajiinamia na muda mfupi baadaye, machozi yalianza kumtoka na kuulowanisha uso wake. Kumbukumbu za penzi lake na Jafet zilikuwa zikipita ndani ya kichwa chake na kumfanya ajisikie vibaya mno.

Mara kwa mara alikuwa akishindwa kujizuia anapomkumbuka Jafet kwani aliona kama moyo wake umedhulumiwa kitu muhimu sana, bado hakutaka kukubaliana na ukweli kwamba hatapata tena muda wa kuwa na Jafet.

Kila alipokuwa anakumbuka ucheshi wake, upole na mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kijana huyo, alikuwa anashindwa kabisa kuzuia machozi yasiulowanishe uso wake.

“Jamani Anna, mbona hivyo? Nisamehe basi, sitarudia tena kukutamkia mambo ya mapenzi,” alisema William kwani alishindwa kabisa kuelewa ni kwa sababu gani msichana huyo alikuwa amebadilika kiasi hicho. Alihisi kwamba huenda amemkwaza sana kwa kumtongoza, hakuelewa kabisa kilichokuwa kinapita ndani ya kichwa chake.

“Naomba nikapumzike, tutaongea kesho,” alisema Anna huku akisimama, machozi yakiwa yanaendelea kumtoka. William alibaki amepigwa na butwaa, akabaki kujilaumu ndani ya moyo wake kwa kumueleza Anna ukweli wa nafsi yake.

***

“Mtoto wenu amewahi kuwa na matatizo ya figo?”

“Hapana ila amewahi kufanyiwa upasuaji wa kutoa figo moja, akamchangia rafiki yake aliyekuwa na matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi.”

“Tatizo limeanzia hapo, inaonesha figo moja aliyobaki nayo ina matatizo, inabidi niwaandikie rufaa ya kwenda Hospitali ya Bugando, hapa hatuna uwezo wa kumtibu.”

“Mungu wangu, sasa itakuwaje dokta?”

“Ndiyo kama hivyo nilivyosema, labda Bugando madaktari bingwa wa figo wanaweza kumsaidia,” alisema daktari baada ya kumfanyia Jafet vipimo na kubaini kilichokuwa kinamsumbua.

Kauli kwamba figo yake moja iliyosalia baada ya kumtolea nyingine Anna ilikuwa na matatizo, ilimchanganya sana mama yake Jafet. Alipotoka kwenye chumba cha daktari alienda kumwambia mumewe aliyekuwa amekaa nje ya chumba cha daktari, naye akaonesha kushtuka mno kusikia matatizo hayo ya mtoto wao.

“Sasa tutafanyaje na pesa hatuna?”

“Tutajua cha kufanya mume wangu, hatuwezi kumuacha mtoto afe kwa sababu hatuna pesa, haiwezekani,” alisema mama yake Jafet huku akijifuta machozi. Kwa kuwa hawakuwa na fedha za kutosha kwa safari ya kuelekea Bugando, ilibidi wakubaliane kurudi kijijini Rwamgasa kwa ajili ya kutafuta fedha za matibabu ya mtoto wao huyo.

Jafet akapewa dawa za kutuliza maumivu na kurudi na wazazi wake mpaka kijijini Rwamgasa.

“Sasa tutafanyaje mke wangu?” baba Jafet alimuuliza mke wake huku akionesha kuchanganyikiwa kabisa na majibu ya daktari. Hata ile tabia yake ya kwenda kukesha kwenye vilabu vya pombe za kienyeji ilibidi aiache kwa muda kutokana na matatizo ya mwanaye.

“Nimepata wazo, unaonaje kama hii nyumba tukiipangisha ili kodi tutakayopata ndiyo tutumie kwa matibabu ya Jafet?”

“Halafu sisi tutaenda kukaa wapi?”

“Tutakaa kwenye lile banda la uani, hakuna namna,” alisema mama yake Jafet, mumewe akatafakari kwa dakika kadhaa kisha akashusha pumzi ndefu na kumgeukia mke wake, akatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana naye.

Hakukuwa na muda wa kupoteza, siku hiyohiyo walianza kuhamisha vyombo vyao vichache kwenda kwenye kibanda kilichokuwa pembeni, ambacho walikuwa wakiishi awali kabla hawajajengewa nyumba hiyo na wazazi wa Anna kama shukrani kwa ajili ya kijana wao kumtolea figo binti yao.

Wakatafuta madalali na kazi ya kutafuta mpangaji ikaanza mara moja. Kwa kuwa nyumba hiyo ilikuwa na mwonekano mzuri, harakaharaka walipata mpangaji, mwalimu wa shule ya msingi ya kijijini hapo ambapo waliingia mkataba na kukubali kumpangisha kwa muda wa miezi sita.

Siku mbili baadaye, safari ya kumpeleka Jafet Hospitali ya Bugando kwa ajili ya vipimo zaidi ilianza.

1 Comment
  1. Frank Jovine says

    Nice xtory

Leave A Reply