The House of Favourite Newspapers

Shoga; Usidanganyike, hakuna penzi la ulozi!

0

Shoga yangu, kufuatia Mwenyezi Mungu kutujalia afya njema na kutuongezea dakika za kuvuta pumzi yake, kila mmoja wetu amshukuru kwa hilo.

Aidha, itakuwa vizuri kama kumshukuru huko kutakwenda sambamba na kuyafanya mambo mazuri aliyotuagiza kupitia vitabu vyake vitakatifu.

Baada ya kusema hayo, sasa ngoja nirejee kwenye mada niliyowaandalia ambayo naamini kwa wengi siyo ngeni kwa sababu imekuwa ikizungumzwa sana na baadhi ya wasanii kuimba.
Shoga, topiki niliyopanga kuzungumza nawe inahusu suala la mapenzi kwamba hayana ulozi isipokuwa mlozi ni mwanamke husika.

Nasema hivyo kwa sababu nawashangaa baadhi ya wenzetu ambao kila kukicha wamekuwa wakisaga soli za viatu kwenda kwa waganga kwa lengo la kuwaroga waume wao ili wawapende na kuwashika.
Shoga yangu, kama umeona mumeo amebadilika anachelewa kurudi nyumbani au lugha zinakuwa gongana ni kujichunguza ili ubaini chanzo maana unaweza kuwa wewe.

Nasema hivyo kufuatia shoga yetu mmoja hivi karibuni kunilalamikia kwamba mumewe kabadilika tabia ghafla hivyo kutaka kwenda kwa kalumanzila kuomba ndumba ya kumtuliza nyumbani.

Aliponiambia hivyo, moja kwa moja nilijua mabadiliko ya tabia ya mumewe yana sababu ndipo nilimwuliza kama mambo aliyokuwa akimfanyia enzi za urafiki, uchumba na siku za mwanzo wa ndoa yao anayafanya yote akasema si yote.

Shoga yangu, unategemea nini kama ujiweki msafi, chumba chenu kinakuwa kichafu, kauli mbali kwa mumeo, baba akitaka chakula cha usiku unamwambia umechoka kama siyo kumpa tiketi ya kutoka nje?
Bila kukuonea huruma atatafuta kiburudisho cha nje na kukuacha ukihangaika kwa waganga na kupoteza fedha nyingi bila mafanikio. Kuwa makini!

Leave A Reply