The House of Favourite Newspapers

Si kwamba hajiwezi faragha, ishu ni we unamsaidiaje?

0

NI Jumanne tena! Jumanne inayochangia kukatika kwa siku kuelekea uchaguzi mkuu mwezi huu. Bado kama siku 11 tu, taifa liingie kwenye kupiga kura kuwachagua, madiwani, wabunge na rais wa nchi.

Tuachane na hayo ya siasa, mimi leo nakuja na mambo yetu ya elimu ya maisha kuhusu mapenzi. Mada yangu ya leo inasema; si kwamba hajiwezi faragha, ishu ni we unamsaidiaje?

Nimeamua kuandika mada hii baada ya kukutana na ndugu mmoja, nafahamiana naye kwa miaka mingi kidogo. Huyu ndugu anasema kuwa, ameoa mwaka jana. Lakini kesi kubwa inayoiweka kizimbani ndoa yake ni yeye kushindwa kumridhisha mkewe kwenye haki yake ya ndoa.

SIKIA USHUHUDA WAKE

“Amekuwa akinishutumu kwamba mimi sijiwezi faragha. Lakini ninavyojijua mimi kwenye eneo hilo niko fiti. Unajua mbaya zaidi ni kwamba, mpaka nafunga naye ndoa hatukuwahi kukutana kimwili, maana yeye alikuwa akiishi Moshi (Kilimanjaro), mimi hapa Dar.

“Hali hii imekuwa ikinipa changamoto kubwa sana. Inawezekanaje? Ina maana mimi sina nguvu za kiume siku hizi? Na kama sina tatizo hii limenianza lini?”

AJIPIMA NJE

“Lakini ili kujiridhisha kwamba bado nipo imara au la! Siku moja nilichepuka kwa makusudi kabisa. Cha ajabu kule nikawa imara sana na kuweza kumudu tena kwa kiwango kinachotakiwa.

“Hali hiyo nayo ilinifanya nihisi kwamba, huenda kuna mtu katuchezea mimi na mke wangu. Kwamba, nikiwa na yeye siwezi, nikiwa na mwanamke mwingine nakuwa imara sana. Da!”

NIKAZUNGUMZA NAYE

Kwa maelezo ya huyu ndugu, nilianza kuzungumza naye mawili matatu nikabaini mambo mawili. Kwanza, kumbe anapotaka kushiriki na mke wake, ni yeye ndiyo anajishughulisha kujiweka tayari. Mke hana habari hiyo.

Hilo nililithibitisha kwa kuniambia mwenyewe. Lakini aliniambia kuwa, huko alikokwenda kujaribu walikuwa wanashirikiana kuwekana sawa. Unaona hapo? Tatizo liko hapa!

NAZUNGUMZA NA WOTE

Hili nataka kulisema kwa wote. Si kwa wanawake tu, hata wanaume pia kwani hii ni tabia. Wengi wanataka kuingia kwenye kutaka kushiriki, wakiamini wao siyo wanaotakiwa kuwaandaa wenzao, bali wenzao kuwaandaa wao. Hii si sawasawa. Unampa mwenzio kibarua kigumu sana cha kukuweka sawa wewe na pia kujiweka sawa yeye.

Kushiriki ni tukio linalotakiwa kusaidiana. Siyo mmoja akiona mwenzake hawezi, anakurupuka na kusema; ‘ooo! Mwenzangu hajiwezi faragha’ wakati kumbe we mwenyewe ukifika huko faragha unakuwa kama mfu anayesubiri kuombewa!

MATOKEO YA TABIA HII

Kuna wengi wanapokutana na lawama hizi za ‘hajiwezi faragha’, awe mwanamke au mwanaume, ikitokea akachepuka na kukutana na anayejua maandalizi hujikuta na yeye anafanya vizuri. Baada ya hapo ni kutengana tu, maana mtu anajiona ameshapata mahali sahihi.

Tuache tabia ya kulaumu ‘mwenzangu hajiwezi faragha’ jiulize kwanza wewe unamsaidiaje? Unapojitupa kwenye sita kwa sita na kutulia kimya kama mti ulioangushwa na mvua bila kujishughulisha kwa nini unamlaumu?

Wataalam wa kisaikolojia wameanika kwamba, vilio vya wanaume wengi kuhusu upungufu wa nguvu za kiume si vya kweli. Wengi wanakumbana na wenzao wao ambao hawajui kuwaandaa na inapotokea akatoka nje na kukutana na ‘wataalam’ mambo huwa supa kabisa.

KUJIEPUSHA NA HILI

Wataalam haohao wanasema kuwa, kama mmoja anajikuta hawezi katika kushiriki, mwenza wake anapaswa kuzungumza naye polepole na si kumkandia au kumkashifu hali ambayo huzidi kumwongezea tatizo la kiakili yule anayekashifiwa.

Tuonane wiki ijayo tayari kwa mada nyingine. 

Leave A Reply