The House of Favourite Newspapers

Siku ya Mazingira Kuadhimishwa Butiama Kesho

0

Na Mwandishi Wetu

TUNAISHI vizuri, tunapata mvua, maisha yanakwenda vizuri kwa sababu ya mazingira. Mazingira ni kitu muhimu sana katika maisha yetu na ndiyo maana kila siku tunaambiwa kwamba hatutakiwi kukata miti au kuchafua mazingira.

Tarehe 5 mwezi Juni mwaka 1972, Baraza la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano wake wa kwanza uliohusu mazingira huko Stockholm nchini Sweden na katika mkutano huo, wakaunda Shirika la kushughulikia mazingira waliloliita United Nations Environment Programme (UNEP) na wakakubaliana kwamba tarehe hiyo kila mwaka itakuwa ni Siku ya Mazingira Duniani.

Makamu wa Rais Bi. Samia Suluhu akizungumza na wanahabari (picha na maktaba)

Ni miaka 45 imepita. Dunia itakwenda kuadhimisha tena siku ya Mazingira Duniani leo na kesho, kimataifa itafanyikia nchini Canada lakini kwa hapa Tanzania, Watanzania wote tutaungana pamoja kuiadhimisha katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara, kijiji ambacho Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alizaliwa na kuzikwa.

 

Sisi kama Watanzania tunatakiwa kuungana pamoja. Si jambo jema kuona watu wakiendelea kuchafua mazingira, kukata miti hovyo huku tukijua kwamba kufanya hivyo kunaweza kuleta hatari katika maisha yetu.

Ni mara nyingi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa January Makamba amekuwa akitukumbusha kwamba sasa ni wakati wa Watanzania kutunza mazingira yetu. Kutunza mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu, si jukumu la yule na huyu bali ni jukumu lako pia.

Ni mara ngapi umekuwa ukiona watu wakikata miti? Ni mara ngapi umeona watu wakichafua mazingira kiholela na kubaki kimya? Mtanzania mwenzangu, unatakiwa kuwa mtu wa kwanza kupaza sauti juu ya mazingira yetu, unatakiwa kuhamasisha watu kupanda miti kwa wingi kwani hata maisha yetu pia huchangiwa na wingi wa miti.

Kumbuka kwamba leo na kesho tutaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara, itakuwa ni kumuenzi Baba wa Taifa kwa jinsi alivyojitolea katika kulinda mazingira yetu. Wewe kama Mtanzania mwenzangu, tuungane kwa pamoja kuiadhimisha siku hii muhimu.

Leave A Reply