The House of Favourite Newspapers

Siku Ya Mazingira Kuadhimishwa Butiama Leo

0

STORI NA MUANDISHI WETU | RISASI JUMAMOSI | HABARI

TUNAISHI vizuri, tunapata mvua, maisha yanakwenda vizuri kwa sababu ya mazingira. Mazingira ni kitu muhimu sana katika maisha yetu na ndiyo maana kila siku tunaambiwa kwamba hatutakiwi kukata miti au kuchafua mazingira. Juni 5, 1972, Baraza la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano wake wa kwanza uliohusu mazingira huko Stockholm nchini Sweden na katika mkutano huo, liliundwa shirika la kushughulikia mazingira, United Nations Environment Programme (UNEP) na wakakubaliana kwamba tarehe hiyo, kila mwaka itakuwa ni Siku ya Mazingira Duniani. Ni miaka 45 imepita sasa.

Dunia itakwenda kuadhimisha tena siku hiyo muhimu leo na kesho, kimataifa itafanyikia nchini Canada lakini kwa hapa Tanzania, maadhimisho yatafanyika katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara, kijiji ambacho Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alizaliwa na kuzikwa. Sisi kama Watanzania tunatakiwa kuungana pamoja.

Si jambo jema kuona watu wakiendelea kuchafua mazingira, kukata miti hovyo huku tukijua kwamba kufanya hivyo kunaweza kuleta hatari katika maisha yetu na vizazi vijavyo.

Mara kwa mara, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), mheshimiwa January Makamba amekuwa akitukumbusha kwamba sasa ni wakati wa sisi Watanzania kutunza mazingira yetu. Kutunza mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu.

Ni mara ngapi umekuwa ukiona watu wakikata miti? Ni mara ngapi umeona watu wakichafua mazingira kiholela na kubaki kimya? Mtanzania mwenzangu, unatakiwa kuwa mtu wa kwanza kupaza sauti juu ya mazingira yetu, unatakiwa kuhamasisha watu kupanda miti kwa wingi kwani hata maisha yetu pia huchangiwa na wingi wa miti. Kumbuka kwamba leo na kesho tutaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara, itakuwa hii itakuwa ni sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa kwa jinsi alivyojitolea katika kulinda mazingira yetu. Wewe kama Mtanzania mwenzangu, tuungane kwa pamoja kuiadhimisha siku hii muhimu kwa vitendo.

Leave A Reply