The House of Favourite Newspapers

SIMBA inakosea wapi? Soma Hapa

Wachezaji wa timu ya Simba wakifanya mazoezi.

MSIMU huu wa 2018/19, Simba ilifanikiwa kutimiza safari yake ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuikosa kwa takribani misimu mitano. Msimu uliopita ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ilishiriki mara ya mwisho msimu wa 2012/2013.

 

Ikiwa chini ya Kocha Mfaransa Pierre Lechantre na msaidizi wake, Masoud Djuma raia wa Burundi, msimu uliopita Simba ikachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kujikatia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Safari yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikaanza hivi; 1.

HATUA YA AWALI Simba ilianza safari yake kwenye michuano ya kimataifa Novemba 28, mwaka jana. Ilianzia hatua ya awali kuvaana na mabingwa wa Eswatini, Mbabane Swallows ambao msimu uliopita walifika hatua ya makundi. Simba ilianzia nyumbani ambapo ilishinda kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

 

Baadaye mechi ya marudiano ilichezwa Desemba 4, 2018 nchini Eswatini na Simba kushinda kwa mabao 4-0 na kufanikiwa kusonga hatua ya kwanza ya michuano hiyo. Hatua iliyofuata Simba ilicheza na Nkana FC ya Zambia ambao katika ligi ya nchi yao, walikuwa washindi wa pili nyuma ya mabingwa Zesco United.

 

Hawa walianza kwao Kitwe Zambia na waliweza kuifunga Simba mabao 2-1. Lakini walipokuja kurudiana hapa Tanzania, mambo yalibadilika na Simba iliweza kuwatandika mabao 3-1. Simba ikafuzu hatua ya makundi na Nkana ikaangukia Kombe la Shirikisho Afrika.

 

2. HATUA YA MAKUNDI Katika makundi, Simba ikapangwa na Kundi D na timu za AS Vita Club ya DR Congo, Al Ahly (Misri) na JS Saoura (Algeria). Hivi sasa tayari Simba imecheza na wapinzani wake wote bado tu mechi za marudiano. Katika mechi ambazo Simba imecheza imevuna alama tatu huku kinara wa kundi Al Ahly akiwa na alama saba.

 

MATOKEO YA SIMBA HATUA YA MAKUNDI Simba 3-0 JS Saoura AS Vita Club 5-0 Simba Al Ahly 5-0 Simba

 

MECHI ZILIZOSALIA Simba vs Al Ahly JS Saoura vs Simba Simba vs AS Vita Club

Katika makundi manne yaliyopangwa kwenye michuano hiyo, timu mbili katika kila kundi ndizo zitafuzu hatua ya robo fainali.

 

3.SIMBA IMEKOSEA WAPI?

Simba mpaka sasa katika kundi lake licha ya kutoburuza mkia, lakini ni wazi imeonekana kuwa na safu butu ya ulinzi ambayo katika michuano hiyo ndiyo timu ambayo imeruhusu mabao mengi zaidi kuliko nyingine. Timu hiyo katika mechi tatu imefanikiwa kufunga mabao matatu tu na ikiruhusu kufungwa mabao kumi. Licha ya kuwa na washambuliaji wazuri kama Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco, lakini wameshindwa kufunga hata bao moja kwenye michezo yao miwili iliyopita.

 

4. JE, WANA NAFASI YA KUVUKA MAKUNDI?

Kwa mechi ambazo Simba imesalia nazo, mbili ni za nyumbani na moja ugenini dhidi ya JS Saoura. Mechi mbili za nyumbani ni dhidi ya Al Ahly na AS Vita Club timu ambazo Simba ilipokwenda kwao iliambulia kipigo sawa cha mabao 5-0.

 

Hivyo Simba inaweza kupata matokeo mazuri au isipate kutokana na uwezo wa timu ambazo inaenda kukutana nazo. Kikubwa ambacho Simba inatakiwa kufanya ni kushinda mechi zake hizo za nyumbani ili kujitengenezea nafasi ya kufuzu hatua inayofuata. Vinginevyo mambo yatakuwa magumu.

 

5. KOCHA NA WACHEZAJI Kwa hali ilivyo sasa ndani ya kikosi cha Simba, kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems anatakiwa kuja na mbinu mpya ambazo zitaweza kuiokoa timu hiyo kupata matokeo hasa safu ya ulinzi pamoja na ushambuliaji.

 

Wachezaji pia nao wanatakiwa kujithimini na watambue majukumu yao na waone umuhimu wa michuano ambayo wanashiriki sio kwenda ilimradi watambue kuwa uwezekaji mkubwa umetumika mpaka hapo walipofika hasa wachezaji wa kimataifa ambao viwango vyao vimeonekana kuwa vya kawaida.

MARTHA MBOMA, Dar es Salaam

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.