The House of Favourite Newspapers

Simba Kukiwasha na AS Vita Leo, Uwanja wa Mkapa

0

UNAAMBIWAzege halilali leo kwani Simba wamepanga kumaliza kabisa hatua ya makundi kwa kuhakikisha wanalamba ushindi dhidi ya AS Vita na kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Timu hizo katika mchezo wa awali uliopigwa katika Jiji la Kinshasa, DR Congo Simba ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Mkongomani Chris Mugalu kwa njia ya penalti.

 

Simba, leo itawakaribisha AS Vita saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu na vijana wa Msimbazi wanahitaji alama moja tu ili watinge robo fainali ya michuano hiyo.

Msimamo wa Kundi A, unaonyesha kuwa Simba wako kileleni wakiwa na alama 10 wakifuatiwa na Al Ahly wenye saba, AS Vita wana nne na Al Merrikh wana moja, timu zote zimecheza mechi nne.

 

Akizungumzia mchezo, Kocha Mkuu wa Simba Mfaransa Didier Gomes alisema maandalizi waliyofanya kuelekea mchezo huo yanawapa matumaini ya kufanya vizuri ikiwemo ushindi.

 

Gomes alisema katika kuelekea mchezo huo wameweka malengo ya kushinda kwani wanajiamini na wana uwezo wa hilo katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ya ushindi.Aliongeza kuwa kikubwa wanataka ushindi ili wajiwekee nafasi nzuri ya kumaliza wakiwa kileleni katika kundi lao.

“Timu yangu haikuwa na mapumziko wakati wa wiki za kimataifa kwani pamoja na kuwa na idadi ndogo ya wachezaji, tuliendelea kufanya mazoezi makali kujiandaa na mchezo huo kwa wachezaji ambao hawakuitwa kwenye timu zao za taifa.

 

“Kikubwa ambacho kinatupa nguvu ya kuamini kwamba tutapata matokeo mazuri mbele ya AS Vita ni hali ya kujiamini na maandalizi mazuri ambayo tumeyafanya.“Katika mchezo huu malengo yetu ni kupata ushindi. Tuko makini na tumeweka malengo ya kushinda.

 

Tunajiamini, tunao uwezo wa kufanya vizuri na kutinga robo fainali mapema,” alisema Gomes.Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa AS Vita, Florent Ibenge mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam, juzi alisema kuwa mchezo huu kwetu tunauchukulia kama fainali ambao ni lazima tushinde.

 

“Tunashukuru tumefika salama, tupo tayari kwa ajili ya mechi yetu ambayo matumaini yetu yote yapo katika mchezo huu, kwetu ni kama fainali tunafahamu haitakuwa kazi nyepesi lakini tupo tayari kwa ajili ya mapambano na hakuna cha zaidi ya hilo.”AS Vita walitua nchini juzi usiku wakitokea DR Congo na kikosi cha wachezaji 24 tayari kwa ajili ya kuwavaa Simba.

Leave A Reply