The House of Favourite Newspapers

Simba Kumenoga Majembe Yatinga Mazoezini

0

SIMBA kumenoga, hiyo ni baada ya majembe yao kuingia kambini jana Jumatano kwa ajili ya kumalizia msimu huu ambao katika Ligi Kuu Bara ndiyo vinara na wapo karibu kabisa kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.

 

Baada ya kuingia kambini jana maeneo ya Ndege Beach nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wakafanyiwa vipimo vyote muhimu ikiwa ni pamoja na corona ili kujua hali zao, kisha jioni wakaanza mazoezi kwenye Uwanja wao uliopo Bunju, Dar.

Aliyeongoza katika vipimo hivyo ni daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe.Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema: “Utaratibu uliopo kwa sasa ni wachezaji kuripoti kambini na kufanyiwa vipimo ikiwa ni pamoja na Corona lengo ni kujua afya zao kabla ya kuanza mazoezi.”

 

Baadhi ya wachezaji ambao jana waliingia kambini asubuhi na mapema ni Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Jonas Mkude, Miraj Athuman, Kennedy Juma, Gerson Fraga, Beno Kakolanya, Tairone Santos, Shomari Kapombe, Said Ndemla na Deo KandaKatika hatua nyingine, viungo wa kimataifa wa timu hiyo, Mkenya, Francis Kahata, Mzambia, Clatous Chama na Msudan, Sharraf Shiboub wapo hatarini kuikosa michezo ya awali ya Ligi Kuu Bara kutokana na kukwama nchini mwao.

Wakati wachezaji hao wakikwama, juzi Jumanne mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere raia wa Rwanda aliwasili jijini Dar akitokea kwao.Mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally ‘Gazza’, alisema kuwa bado hawajafahamu hatma ya viungo wao hao kutua nchini kujiunga na wenzao kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ligi iliyopangwa kurejea kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.

 

“Wachezaji watatu pekee ndiyo bado hawajaripoti kambini ambao uwezekano wao kuwahi michezo ya awali ya ligi ni mdogo, licha ya uongozi kupambana kuhakikisha wanawahi kama ilivyokuwa kwa Kagere.

“Kahata nchini kwao mipaka ya mikoa imefungwa, hivyo ni ngumu kwake kutoka sehemu moja kwenda nyingine, pia Shiboub nchini kwao bado hawajaanza kuruhusiwa kutembea mitaani muda wote wapo ndani kutokana na Corona, kidogo Chama kuna matumaini ya kuwahi ingawa bado hatujajua atakuja lini,” alisema Gazza.

STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA NA WILBERT MOLANDI, DAR

Leave A Reply